Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwasha umeme kwenye Zahanati ya kijiji cha Mkalama, wilayani Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19, 2020 huku akishuhudiwa na viongozi wachache ikiwa ni hatua ya kuepuka mikusanyiko ya wananchi ili kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kulia) na Ujumbe wake, wakiangalia nguzo za umeme zilizorundikwa chini akiwa katika ziara ya kazi eneo la Kiomboi, Singida, Aprili 19 mwaka huu. Waziri aliagiza kuondolewa kwa nguzo hizo mara moja, zisimikwe na kuwaunganishia umeme wananchi wa eneo hilo
 
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mbele-kulia) akiwa amefuatana na viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Milade, Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19 mwaka huu. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka na wa kwanza kulia ni Mbunge wa Mkalama, Allan Kiula.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto), akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini wilayani Iramba, kufunga nyaya za umeme katika nguzo alizosimika katika Kijiji cha Msingi na kuwaunganishia umeme wananchi ndani ya siku saba. Alitoa agizo hilo Aprili 19 mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka (kulia) akitoa salamu za ukaribisho kwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (anayesaini kitabu), baada ya Waziri kuwasili wilayani humo kwa ajili ya ziara ya kazi, Aprili 19 mwaka huu. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Mkalama, Allan Kiula.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kushoto), akisalimiana na viongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, alipowasili wilayani humo Aprili 19, 2020 kwa ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19, 2020. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Mkalama, Allan Kiula na wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Jackson Masaka.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mbele) na Ujumbe wake, wakiwa katika ziara ya kazi wilayani Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19 mwaka huu. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka.



Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewasha umeme katika maeneo kadhaa ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida na kusisitiza viongozi wa wilaya, vijiji na vitongoji kutoa kipaumbele kwa taasisi za umma zilizo katika maeneo yao ili ziunganishiwe nishati hiyo muhimu.
Akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo, Aprili 19 mwaka huu, Dkt Kalemani alibainisha kuwa kipaumbele cha Serikali kupeleka umeme vijijini ni katika kuhakikisha taasisi zote za umma zinakuwa na umeme ili kuziwezesha kutoa huduma bora zaidi.
Alisema kuwa, Rais John Magufuli ametoa pesa nyingi kwa lengo la kupeleka umeme vijijini, hivyo ni lazima fedha hizo zitumike kwa busara katika kukidhi mahitaji ya wananchi walio wengi, hususan katika kuboresha huduma za afya, elimu, maji, kilimo pamoja na uanzishwaji viwanda vidogo vidogo.
“Ndugu zangu viongozi, nawasisitiza mhakikishe taasisi zote za umma katika maeneo yenu zinalipiwa gharama ya kuunganisha umeme ambayo kwa vijijini ni shilingi elfu 27 tu ili ziunganishiwe nishati hiyo na hivyo kuboresha huduma.”
Akizungumza kwa nyakati tofauti na viongozi wa vijiji vya Milade na Mkalama baada ya kuwasha umeme katika Zahanati za vijiji hivyo, aliwapongeza kwa kuona umuhimu wa kulipia gharama za umeme zilizowezesha kuunganishiwa nishati hiyo na kuwataka viongozi wengine wa vijiji na vitongoji nchini kote kuiga mfano huo.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani alitoa muda wa siku saba kwa Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, wilayani Iramba, kuvuta nyaya na kuwaunganishia umeme wananchi katika kijiji cha Msingi.
Waziri alitoa agizo hilo baada ya kushuhudia nguzo zilizosimikwa kwa muda mrefu pasipo kufungwa nyaya wakati akipita eneo hilo akitokea Mkalama.
Alimtaka Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu ambaye alifuatana naye katika ziara hiyo kumchukulia hatua Mkandarasi husika endapo hatatimiza agizo hilo.
Aidha, akiwa eneo la Kiomboi, Waziri alitoa siku tano kwa Mkandarasi husika kuhakikisha anaondoa nguzo za umeme zilizorundikwa chini na kuzitumia kuwaunganishia umeme wananchi wa eneo hilo.
Akiwa ameoneshwa kukerwa na hali hiyo ya nguzo kurundikwa wakati wananchi wa eneo husika hawana umeme, Waziri alimwagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Singida, Abdulahaman Nyeye kumchukulia hatua Meneja wa Shirika hilo wilayani Iramba, endapo atashindwa kusimamia utekelezaji wa agizo lake.
Pia, alimwagiza Mkuu wa Wilaya husika kumchukulia hatua za kisheria Mkandarasi husika endapo hatatekeleza agizo lake ikiwa ni pamoja na kumweka ndani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka, aliipongeza Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kutekeleza kikamilifu ahadi zake kwa wananchi, ikiwemo upelekaji umeme vijijini.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Allan Kiula, alimpongeza Waziri wa Nishati na Naibu wake Subira Mgalu kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Vilevile, alimwomba Waziri Kalemani kufikisha salamu za shukrani kwa Rais Magufuli kutokana na upendeleo ambao amekuwa akiwapatia katika kuwapelekea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo umeme.
Hadi sasa jumla ya vijiji 57 vya Wilaya ya Mkalama kati ya 70 vilivyopo, vimekwishafikishiwa nishati ya umeme. Waziri Kalemani ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 2021, vijiji vyote vitakuwa vimekwishapelekewa umeme.
Waziri Kalemani ameendelea kusisitiza kuwa katika kipindi hiki ambacho Taifa linakabiliana na ugonjwa wa Corona, ziara zake kukagua miradi katika maeneo mbalimbali hazitahusisha wananchi ili kuepuka mikusanyiko. Badala yake, ziara zitahusisha viongozi wachache wa vijiji na vitongoji katika maeneo husika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: