Na John Walter-Manyara

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa(Takukuru) mkoani Manyara imeeleza namna ilivyokisaidia chama cha wachimbaji wadogo wa madini(MINASCO) kukusanya madeni kutoka kwa watu waliokopa na kudumu na fedha zao kwa muda mrefu.

Akizungumza na waandishi wa Habari Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoani hapa Isdory Kyando, alisema katika ufuatiliaji wao walibaini chama hicho hakina fedha kabisa kwenye akaunti yao ila kinawadai wanachama wake sh. Mil. 58.

"Fedha hizo ambazo chama kilikuwa kinawadai wanachama wake ni madeni sugu yaliyokuwa yameshindikana kulipwa kwa utaratibu wa kawaida,"Alisema Kyando
Aidha alisema madeni hayo ni ya muda mrefu tangu mwaka 2018 lakini Takukuru waliendelea kufatilia madeni hayo toka Machi, 2020 kupitia ofisi zao za Simanjiro.

Alisema walikusanya sh. Mil. 19 ambapo fedha hizo waliziweka kwenye akaunti maalum ili zoezi la ukusanyaji likikamilika wakabidhiwe viongozi wa Minasco.
Alifafanua kuwa kwa utaratibu wa sheria za madini leseni za chama hicho kwa migodi 14 zilikuwa zimeisha tangu Januari 2020.

"Hivyo wachimbaji hao wadogo ilipaswa wanyanganywe migodi hiyo yote, tukiwa tunaendelea na ukusanyaji wa fedha hizo tulipata taarifa kutoka kwa mrajisi wa vyama vya ushirika kuwa chama hicho kinadaiwa,"Alieleza
Alisema mrajisi aliiambia Takukuru kuwa wanadaiwa sh. Mil. 14.5 na ofisi ya madini na kwamba kama hawatalipa fedha hizo watanyang'anywa migodi yote.

Kyando alisema kutokana na mazingira hayo ni busara kuwakabidhi fedha hizo na wasimamie kuhakikisha zinakwenda kulipa deni la leseni ili hawa wachimbaji wazawa waendelee kukaa kwenye ajira na kunufaika na rasilimali za nchi yao.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wanachama wa vyama vya ushirika kurejesha mikopo wanayopewa kwa wakati.
Naye mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani hapa Venance Msafiri alikiri sh. Mil. 14.5 kurejeshwa na wadaiwa sugu ambazo zinaenda kulipia leseni za wachimbaji hao.

Msafiri alisema operesheni ya kufatilia fedha za vyama vya ushirika itaendelea siyo kwamba imeishia happy hivyo cha msingi wanaodaiwa wanatakiwa kuzirejesha fedha.
Aliongeza kuwa ubadhilifu wa fedha na mali za ushirika umepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Kwa upande wake mjumbe wa Bodi ya Minasco Curtius Msosa alisema kwa hatua hiyo waliyoichukua Takukuru kwa kushirikiana na Ofisi ya mrajisi kukusanya madeni imewapa faraja.
Msosa alisema sasa itawasaidia kufanya shughuli za maendeleo na kupiga hatua huku akidai watanufaika na madini na siyo kubaki kuangaika na watu wanaodidimiza ushirika kwa kukopa bila kurejesha fedha.

Chama hicho cha wachimbaji kinadaiwa kuwa na wanachama 50 ambapo kila mtu anachangia asilimia tano ya madini wanayochimba na ikitokea wengine wakatoa taarifa ambazo siyo sahihi viongozi wanatafuta takwimu za serikali ndio zinaonenesha kila mtu amepata kiasi gani cha madini.

Hatua hiyo  ya Takukuru ni katika kutekeleza maagizo ya Rais John Pombe Magufuli kwenye ufuatiliaji na usimamiaji wa urejeshwaji wa fedha za vyama vya ushirika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: