Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akitangaza taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya vyanzo vya ndani vya halmashauri kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020.



Charles James, 

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam limeongoza kundi la halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 78 ya makisio ya mwaka huku Jiji la Dodoma likiwa la mwisho katika kundi la majiji kwa kukusanya asilimia 55 ya makisio yake ya mwaka.

Akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma alipokua akitangaza taarifa za mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo amesema Jiji la Dodoma limeongoza kundi la halmashauri za majiji kwa kukusanya Sh Bilioni 36.04 huku Jiji la Dar es Salaam likiwa la mwisho kwenye kundi hili kwa kukusanya Sh Bilioni 8.

Kwa upande wa halmashauri za miji kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020, Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa mapato ambapo imekusanya Sh Bilioni 7.02 huku Halmashauri ya Mji wa Mbulu ikikusanya Sh Milioni 671.8.

Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imeongoza katika kundi la halmashauri za wilaya kwa kukusanya Sh Bilioni 5.78 huku Halmashauri ya Wilaya ya Gairo ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya Sh Milioni 343.70.

Manispaa ya Iringa imeongoza kundi la halmashauri za Manispaa ambapo imekusanya asilimia 100 ya makisio yake na katika kundi hilo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi imekua ya mwisho kwa kukusanya asilimia 49 kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Waziri Jafo ameitaja Halmashauri ya Mji wa Njombe kuwa imeongoza kwa kukusanya asilimia 130 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2019/20 ambapo halmashauri ya Mji wa Handeni imekua ya mwisho kwa kukusanya asilimia 43.

"Kwa kigezo cha wingi wa mapato Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa kukusanya Sh Bilioni 126.77. Mkoa wa mwisho ni Rukwa ambao umekusanya Sh Bilioni 6.34. Mkoa wa Njombe wenyewe umefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kukusanya asilimia 87 ya makisio ya halmashauri za mkoa huo huku Simiyu ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 51," Amesema Jafo.

Amesema uchangiaji wa fedha za ndani katika shughuli za maendeleo umezigawa halmashauri hizo katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni halmashauri zinazochangia asilimia 60 na kundi la pili ni linalochangia asilimia 40 ya mapato ya ndani.

Uchambuzi unaonesha kundi la kwanza lina halmashauri 16 zinazotakiwa kuchangia asilimia 60 katika miradi ya maendeleo ambapo Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeongoza kwa kuchangia asilimia 38 na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imekua ya mwisho kwa kuchangia asilimia 22 ya mapato yasiyofungiwa kwenye miradi ya maendeleo.

Aidha Jiji la Dodoma limeongoza kwa kuchangia fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ambapo hadi Machi  2020 jiji hilo limechangia Sh Bilioni 20.95.

Katika kundi la pili lenye halmashauri 169 zinazotakiwa kuchangia asilimia 40, Halmashauri ya Uvinza imeongoza kwa kuchangia asilimia 47 ya mapato yasiyofungiwa na Halmashauri za mwisho ni Chamwino, Bumbuli, Nzega, Mafia ambazo zimechangia kwa asilimia 2 ya mapato yasiyofungiwa.
Share To:

Post A Comment: