Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
SEKTA ya Uchukuzi inatoa mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo ya uchumi na pia ni mwezeshaji mkubwa wa sekta za uzalishaji, biashara na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la kitaifa na  kimataifa.

Usafirishaji wa bidhaa na huduma katika masoko, hutegemea zaidi mfumo wa uchukuzi wenye tija na ufanisi kwa ajili ya uhimizaji na uwezeshaji wa biashara na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuokoa muda.

Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa Mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi, ambapo katika miaka ya hivi karibuni umekuwa na kasi kubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Lindi una jumla ya wakazi 864,652, huku nusu ya wakazi hao wakiishi katika maeneo ya pembezoni kuzunguka bahari ya Hindi na wananchi hao kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za kijamii kutokana na maeneo hayo kukosa  usafiri wa uhakika.

Miongoni mwa maeneo yaliyokuwa yakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri ni Kijiji cha Kitunda kilichopo Manispaa ya Lindi ambao awali wananchi wake walikuwa wakitumia vyombo visivyo salama vya usafiri ikiwemo mitumbwi, ngalawa na majahazi kwa ajili ya kuingia na kutoka eneo la Manispaa ya Lindi kutafuta huduma za kijamii.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ilitekeleza ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli aliyoitoa kwa wananchi wa Manispaa ya Lindi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, ilijenga kivuko cha M.V Kitunda kinachotoa huduma ya usafiri wa abiria, magari na mizigo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na MAELEZO, Meneja wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Locky Sabigoro anasema kivuko hicho kilianza kazi rasmi mwezi Machi 2018, ambapo Serikali ilifanya  maboresho ya miundombinu mbalimbali yenye thamani ya Tsh Bilioni 2.2.

Aidha Sabigoro anasema kati ya fedha hizo, kiasi cha Tsh Bilioni 1.9 zimetumika kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara ya kuingilia katika eneo la Kivuko na Tsh Milioni 333 zimetumika kwa ajili ya kujenga maegesho na barabara na kuongeza kuwa Serikali imetumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya uhakika ya kivuko.

Mhandisi Sabigoro anasema kivuko cha M.V Kitunda kina uwezo wa kubeba abiria 100 na mizigo yenye uzito wa tani 50 pamoja na magari sita kwa wakati mmoja na inatumia muda wa dakika 10 hadi 12 tofauti na wakati wa nyuma ambapo walikuwa wanatumia zaidi ya saa 1 kwa ajili ya kuvuka kuelekea upande wa pili.

‘’Kivuko hiki cha M.V Kitunda kina uwezo wa kubeba abiria 1800 kwa siku lakini kwa idadi ya wakazi waliopo katika eneo la Kitunda-Manispaa ya Lindi unakuta kivuko kinabeba abiria 500-600 kwa siku, tumeongea na Serikali ya Mkoa kuona namna bora ya kujenga vivutio vya uwekezaji’’ alisema Mhandisi Sabigoro.

Akifafanua zaidi Sabigoro anasema Serikali ya Mkoa tayari imeanza maandalizi ya kujenga miundombinu ya huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi  wa shule na vyuo vya elimu ya juu katika Eneo la Kitunda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa kijiji cha Kitunda na kurahakisha kasi ya ukuaji wa maendeleo ya Mkoa wa Lindi.

Mhandisi Sabigoro anasema hapo awali hali ya mawasiliano ya usafiri baina ya wananchi wa Kitunda na Manispaa ya Lindi haikuwa nzuri kwani wakazi wa maeneo hayo walilazimika kutumia mitumbwi na maboti kwa  ajili ya kuvuka  upande wa pili kwa ajili ya kupata huduma muhimu za kijamii, ambazo nyingi zinapatikana eneo la Manispaa ya Lindi.

Anaongeza kuwa kwa sasa wananchi wanafurahia huduma ya kivuko cha MV Kitunda kutokana na kutumia muda mfupi kuvuka katika eneo hilo, hivyo TEMESA Mkoa wa Lindi imejipanga kuhakikisha kuwa inalinda miundombinu ya kivuko hicho ili kuleta maendeleo endelevu kwa ustawi wa wananchi wa Manispaa ya Lindi.

‘’Mhe. Rais aliona namna watu walivyokuwa wakihangaika hususani akina mama, walikuwa wakidhalilika sana na wakati ule magari yalikuwa yanazunguka upande wa pili wa eneo la mnazimmoja na kusafiri umbali wa kilometa 70 kuingia eneo la Kitunda, lakini kwa sasa hali ni tofauti usafiri umekuwa rahisi na kutoa unafuu mkubwa kwa wananchi’’ alisema Mhandisi Sabigoro.

Wananchi mbalimbali wa Manispaa ya Lindi wamempongeza Rais Dkt. John Magufuli na serikali ya awamu ya tano kwa kuendelea kutimiza ahadi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ikiwemo ujenzi wa kivuko cha M.V Kitunda ambao utasaidia kuondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati ya Manispaa ya Lindi na kijiji cha Kitunda.

Bi. Subira Hamisi Mkazi wa Manispaa ya Lindi anasema kabla ya kivuko cha M.V Kitunda hali ya usafiri baina ya kijiji cha Kitunda na Manispaa ulikuwa mgumu, na vyombo vya usafiri vilivyotumika havikuwa na utaratibu maalum, lakini kwa sasa hali ni tofauti wanasafiri muda wote na kivuko kinachotumika kina usalama wa uhakika.

Tunapoingeza Serikali kwa kuondoa changamoto ya usafiri kwetu sisi wakazi wa Manispaa ya Lindi, kwa hapo awali ndugu zetu hususani akina mama walikuwa wanapata matatizo mbalimbali pindi walipokuwa wanatumia mitumbwi na maboti ambayo hayakuwa na uhakika wa kupatikana kwake pale ilipokuwa ikihitajika’’ alisema Subira.

Naye Bw. Mohamed Nguse Mkazi wa Kijiji cha Kitunda anasema Kivuko cha M.V Kitunda kimesaidia kuondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati ya Kijiji cha Kitunda na Manispaa ya Lindi na kuinua kipato cha wananchi wa maeneo hayo, kiuchumi na kijamii kwa kuwa Serikali imeanza ujenzi wa vivutio vya uwekezaji vinavyoharakisha ukuaji wa Mji huo na Mkoa wa Lindi kwa ujumla.

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha kuwa kivuko hicho kinaendelea kutoa huduma bora, aliwaomba wananchi wote kuhakikisha kuwa kivuko hicho kinatunzwa vizuri huku huku wakizingatia usalama wa abiria na mali zao, huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa kivuko hicho.

Kwa upande wake Bi Saidika Nanjemela wa Kijiji cha Kitunda, Manispaa ya Lindi alisema kivuko cha M.V Kitunda ni mkombozi wa uhakika wa usafiri kwa wananchi wote wa Manispaa ya Lindi kwa kuwa utatoa fursa ya kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo ambao ndiyo msingi wa maisha ya wananchi wengi wa vijijini.

Uwepo wa kivuko cha M.V Kitunda katika Manispaa ya Lindi,  fursa kwa wananchi kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo ili kujiongezea kipato na kujikwamua na umaskini kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.

Ni wajibu wa wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizo ili kuweza kutoa hamasa kwa serikali kuongeza juhudi katika kubuni mikakati, mipango na sera mbalimbali zitakazosaidia kuharakisha kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: