Monday, 16 March 2020

WAZIRI JAFO AKAGUA UJENZI HOSPITALI YA UHURU, AAGIZA KUONGEZWA KWA NGUVU KAZI


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akitoa maelekezo baada ya kufika kujionea maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru inayojengwa kwa maelekezo ya Rais Dk Magufuli wilayani Chamwino, Dodoma.
 Mafundi wakiendelea na ujenzi wa Hospitali ya Uhuru inayojengwa wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akiwa kwenye ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru wilayani Chamwino, Dodoma.

Charles James, MsumbaTV
WAZIRI  wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya Hospitali ya Uhuru inayojengwa kwa maelekezo ya Mhe Rais Dk John Magufuli katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Mhe Jafo amesema amefanya ziara hiyo maalum ya kukagua ujenzi wa Hospitali hiyo ili kuona hatua ambazo zimefikiwa huku akiwaambia wahandisi wanaosimamia ujenzi huo kutoka TBA na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwa ujenzi huo umechelewa.

Amesema pamoja na mvua kunyeesha lakini bado kasi ya ujenzi huo imekua hairidhishi kutokana na idadi ndogo ya nguvu kazi ambayo imeletwa hapo kutoka JKT.

" Najua tumekua na changamoto ya mvua lakini ndugu zangu hata nyie wenyewe mkiangalia idadi ya Vijana walioletwa hapa kwa ajili ya kazi mtaona ni ndogo na haiendani na aina ya ujenzi unaofanyika hapa.

Niwaagize sasa kuongeza vijana wa JKT. Siyo tu mlete vijana wa kusaidia ujenzi lakini muongeze ambao ni mafundi kabisa ili shughuli hii iweze kwenda kwa kasi na kufikia malengo ya kukamilika ifikapo Mei mwaka huu," Amesema Mhe Jafo.

Waziri Jafo amesema kesho asubuhi atarudi tena kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa maagizo yake ya kuongezwa idadi ya watu kwa ajili ya nguvu kazi.

" Kesho saa mbili na nusu nitakua hapa tena kuangalia utekelezaji wa agizo langu na utofauti wa kazi unavyoenda, mvua inanyeesha lakini tukipata muda kama hivi leo mvua haijanyeesha basi muongeze spidi zaidi, lengo letu ni kuona tunakamilisha katika muda tuliopanga," Amesema Jafo.

Hospitali ya Uhuru wilayani Chamwino inajengwa baada ya Rais Magufuli kuelekeza kufanya hivyo katika sherehe za Uhuru mwaka 2018 na kuelekeza fedha zilizokua zitumike kwenye maadhimisho ya sherehe hizo kujenga Hospitali hiyo mkoani Dodoma.

No comments:

Post a comment