Tuesday, 24 March 2020

WATOTO CHINI YA UMRI WA MIAKA SABA WANAHITAJI KULINDWA NA BABA NA MAMA

Ongezeko la kutelekeza  watoto wenye umri chini  ya miaka saba  limezidi kuchukua sura mpya  katika  mkoa  Tanga  ambapo  takwimu zinaonyesha   kutoka mashauri 115 kwa mwaka 2017/2018 hadi kufikia  387  kwa mwaka  2018/ 2019.
Kwa mujibu wa Ofisa  Ustawi  wa Jamii  Mkoa wa Tanga  Mmasa  Malugu alisema  ongezeko  hilo limeendelea  kushamili  kutokana  na sababu mbalimbali  kitu  ambacho  kinapelekea  watoto hao kukosa  ulinzi  na   usalama  katika  makuzi yao .
Taarifa hizo zimeendelea kuonyesha kuwa mwaka 2016 / 2017 walipokea dawatini kwao  mashauri  262 kati   ya kesi hizo  49 zilipelekwa  mahakanii .
Ofisa Ustawi huyo  amesema  kuwa  vitendo vya  kutelekeza  watoto  ni miongoni  mwa unyanyasaji  wa kijinsia  ambao  wanafanyiwa  watoto wenye umri huo wa chini  ya  miaka  saba  jambo  ambalo  kwa asilimia kubwa  watoto  hao wanakosa  malezi ya baba na mama.
Alieleza   kuwa  baada ya kuona tatizo hilo  linazidi  kushamiri, Mkoa umeamua kujikita katika kuhakikisha miongozo inayotolewa na serikali kuhusu malezi inafuatwa  kama kuanzisha  kamati  za MTAKUWA ambazo zinakuwa  ngazi ya vijiji , mtaa , kata halmshauri na Mkoa,  kwa ujumla.
Mulugu  Alisema  kuwa  lengo la kuanzisha  kamati  hizo  ni kutaka  kusaidia katika malezi, makuzi   pamoja  na kuhakikisha manyanyaso kwa watoto  yanapungua  kwa kiasi kikubwa katika  maeneo ambayo zipo kamati  hizo. Aliongeza kuwa  kamati  hizo  ni mchanganyiko  wa watalaam mbalimbali na  jamii ambao wanakuwa pamoja .
Ingawa haijaelezwa Kwa ni wilaya gani inayoongoza  kwa  matukio  kama vile ya unyanyasaji, ukatili wa kimwili, kingono na kihisia. “Kiukweli,  kesi  nyingi tulizonazo  zinatokea  katika maeneo ya Pwani  kama vile Mkinga , Pangani  na katika shule zilizopo ndani ndani  na hii inatokana na mifumo tuliyonayo sasa,” alieleza Malugu.
Hata hivyo kuetelekeza ni pamoja  na  kutotoa  matumizi  kama  chakula, mavazi , matibabu, makazi,  na  mahitaji  ya  msingi kama  ada  za shule, vifaa  vya  shule  na  kila  kitu  ambacho  ni mahitaji  ya  msingi  kwa  makuzi  na ustawi  wa  mtoto.
Akitoa Takwimu kwenye kongamano la wadau wa ukatili dhidi ya watoto lililofanyika Mkoani Tanga hivi karibuni  , Mkurugenzi  wa Idara  ya Maendeleo ya Watoto katika Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto  Mwajuma Magwiza, alisema takwimu za jeshi la Polisi mwaka 2018 zinaonyesha kuwa mkoa wa Tanga unaongoza kwa kuwa na visa 1039. Mkoa wa Mbeya  unashika nafasi ya pili kwakuwa na visa 1017 .
Prisca  Mwakasindile, ambaye ni Muuguzi katika  kituo cha kulelea  watoto wenye ulemavu kilichopo Jijini Tanga  cha YDCP amesema  kuwa wamekuwa  wakikutana  na changamoto mbalimbali  za watoto wenye  ulemavu  kutelekezwa  na baba  zao kutokana  na hali zao .
Martin Mhina  Mkazi wa Korogwe amesema  kuwa  jambo la kutelekeza  watoto si jambo  jema  na hiyo  inasabishwa na wazazi kukwepa  majukumu yao  pamoja  na  malezi  yao wenyewe. Alisema kuna wanaume  wamejipa  majukumu ya kutafuta watoto lakini bado wao  wanakula  kwa wazazi wao.
Mzazi  mwingine  alijitambulisha  kwajina la Dege Masoli  mkazi wa songe  kilindi amesema kuwa  sababu  inayosababisha  watoto  kutelekezwa  inatokana na  migogoro  ya kifamilia , kukosekana kwa uaminifu  katika  mahusiano  na hali ngumu za  kiuchumi . 
Mwisho..Habari na Rais Saidi Tanga

No comments:

Post a Comment