Monday, 16 March 2020

TAKUKURU ARUMERU YAOKOA MAMILIONI YA FEDHA ZA SACCOS


Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha Frida Weresi akizungumza na waandishi wa habari juu ya chunguzi mbalimbali zinazohusiana na vyama vya ushirika AMCOS na SACCOS Mkoani Arusha.
Na.Vero Ignatus, MsumbaTv

Taasisi ya kupambana na Rushwa mkoani Arusha Takukuru imeendelea kufanya chunguzi mbalimbali zinazohusiana na vyama vya Ushirika (AMCOS na SACCOS) kutokana na malalamiko wanayoyapokea kutoka katika vyanzo mbalimbali na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya viongozi na wanachana hivyo kupelekea baadhi ya vyama vya ushirika kufa au kujiendendesha kwa kusuasua.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha Frida Weresi alisema chunguzi ambazo zinaendelea ili kuwachukulia hatua za kisheria wale wote ambao watakaobainika kutenda makosa ya kijinai na taasisi hiyo inaendeleza kazi ya kuwafuatilia na kuwataka wote waliokopa fedha pasipo kufuata utaratibu au wadaiwa sugu kuhakikisha wanarejesha fedha .

Weresi alisema kuwa Takukuru wilaya ya Arumeru ni mojawapo ya ofisi ambayo inaendelea na chunguzi za vyama vya ushirika na vyama ambavyo vinachunguzwa ni Arumeru Teachers Saccos,Ngurdoto Saccos na Kuwawayata Saccos,kwa muktadha huo wameweza kuokoa kiasi cha shilingi 45,823,205 ambacho kilikuwa ni mikopo iliyotolewa bila utaratibu.

Alisema chama cha Ngurdoto Saccos kwa jitihada za Takukuru kimeweza kurejeshewa kiasi cha shilingi 24,830,350 kati ya shilingi 66,670,450 ambapo Teachers Saccos kimeweza kurejeshewa kiasi cha shilingi 16,981,000 kati ya 31,400,000,kwa upande wa Kuwawayata Saccos kimeweza kurejeshewa sh.4,011,855 kati ya 81,000,000 fedha zote zimeokolewa na kurejeshwa katika akaunti za vyama husika.

Aidha mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha Frida Weresi ametoa wito kwamba yeyote anayejua ni mdaiwa sugu au amekopa pasipo kufuata utaratibu ahakikishe anarejesa pesa hizo la sivyo Takukuru haitakuwa na huruma dhidi yake.

Amesisitiza kwamba pesa zitakazorejeshwa zitumike kwa malengo kusudiwa kwa mustakabali wa ustawi wa vyama na si vinginevyo kwani atakayebainika kwenda kinyume na utaratibu sheria zilizopo Takukuru haitasita kumchukulia hatua

Mkuu huyo wa Takukuru amesisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu kwa mwananchi yeyote yule aliye taarifa za kuwepo kwa ubadhirifu wa vyama vya ushirika na VICOBA asisite kutoa Taarifa Takukuru ili ziweze kufanyiwa kazi.

Kwa upande wake Emmanuel Sanka mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Arusha ametoa wito kwa vyama vya ushirika na vuongozi wao kuhakikisa kwamba kama kuna yeyote yule alikopa fedha na hakuweza kuzirejesha kwa wakati atambue kuwa wameamua kushirikiana na Takukuru kuakikisha fedha hizo zinapatikana na zinarudi sehemu husika

Sanka alisema kuwa waliweza kutoa taarifa za vyama sita mwanzoni na zingine zinaendelea hadi mwishoni mwa mwezi watakuwa wamekamilisha taarifa hizo ili waweze kukabidhi kwa Takukuru kwani watakapomaliza awamu hii waliyoianza watakwenda kwenye awamu nyingine ya uchunguzi ili kufahamu maeneo yapi yana shida

No comments:

Post a comment