Friday, 6 March 2020

MWEKEZAJI KIWANDA CHA PARACHICHI MUFINDI AIPONGEZA SERIKALI ,RC HAPI ATAKA IRINGA WALIME PARACHICHI...

Mwekezaji wa kiwanda cha Parachichi Mufindi Joson Fournier wa pili kulia akitoa maelekezo kwa mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi 
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi na viongozi mbali mbali wakitazama shamba la Parachichi 
Mkurugenzi Mufindi Netho Ndilito akimfungulia mlango wa gari mkuu wa mkoa wa Iringa 

Mkuu wa mkoa wa Iringa akiwa kwenye gari maalum akikagua shamba la Parachichi 
MWEKEZAJI wa kiwanda cha Parachichi kijiji cha Kibidula wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa Joson Fournier ameipongeza serikali kwa kusogeza umeme katika kiwanda hicho .

Akitoa pongezi hizo jana wakati wa ziara ya mkuu wa Iringa Ally Hapi ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi ,mwekezaji huyo alisema pamoja na uwekezaji mkubwa alioufanya katika eneo hilo kwa kulima heka zaidi ya 500  za Parachichi na kujenga kiwanda cha kusindika Parachichi ila changamoto kubwa ilikuwa ni umeme .

"Niipongeze sana serikali sikivu ya Tanzania chini ya Rais Dkt John Magufuli kwa kusikia kilio chetu na kutuletea umeme wa uhakika katika kiwanda chetu pia nampongeza waziri wa Nishati na wewe mkuu wa mkoa kwa ukaribu wenu"

Alisema mwekezaji huyo kuwa kiwanda hicho kinatarajia kuanza kazi mwezi Julai mwaka huu na kitakuwa na uwezo wa kusindika Parachichi tani 14,000 kwa mwaka.

Huku upande wa ajira kiwandani  wananchi zaidi ya 60 watanufaika na ajira za kudumu na wananchi zaidi ya 350 watanufaika na kazi za vibarua kwenye mashamba ya Parachichi .

Alisema soko la Parachichi ni kubwa nchi za Ulaya na kiwanda chake kitasafirisha Parachichi kwenda kuuzwa kwenye soko la Ulaya kwa kupitia uwanja wa Ndege wa Iringa .

Hivyo alitoa Rai kwa wananchi wa mkoa wa Iringa na Njombe kuchangamkia fursa ya kilimo cha Parachichi kwani mashamba ya kiwanda hicho pekee hayawezi kutoshereza uhitaji wa soko la ulaya.

Aidha alisema kuwa kiwanda  kimeendelea na mchakato wa kuzalisha mbegu za kisasa watakazoziuza kwa wananchi kwa gharama nafuu na tayari kuna miche ya kutosha ya kuuzia wananchi wenye uhitaji .

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Hapi alipongeza jitihada za mwekezaji huyo katika uwekezaji mkubwa alioufanya kwani utakuza uchumi wa mkoa na Taifa .

Hata hivyo aliwataka wafanyakazi watakaopata kazi na wale wanaofanya kazi katika kiwanda hicho kufanya kazi kwa uaminifu na juhudi kubwa na kuachana visingizio visivyo na tija vya kukwepa kufika kazini .

Kwani alisema kutokana na uvivu wa baadhi ya watanzania katika kazi kuna uwezekano mkubwa wa Tanzania kuendelea kukosa kuingia katika soko la ushindani wa ajira Afrika.

"Hivi unakuta mtu anaomba ruhusa kazini eti amefiwa na bibiake wa bibi mzaa bibi ama Shangazi yake ana uvimbe mguuni hatukatai kushiriki misiba ya familia ila misiba mingine lazima tukubali kuwakilishwa na wengine twende kwenye uzalishaji mali "alisema Hapi .

Kuhusu umuhimu wa wawekezaji ndani ya mkoa huo aliagiza Halmashauri kutenga maeneo ya uwekezaji na pale mwekezaji anapopatikana basi huduma muhimu zipelekwe kwa wakati .

Wakati huo huo mkuu wa mkoa ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Iringa kujikita katika uwekezaji wa kilimo cha Parachichi kwani ndicho kitakachokuja kuwakomboa vijana wengi baadae .

Kuhusu watumishi wa umma aliagiza kila mtumishi kuwa na shughuli ya kiuchumi nje ya ajira ya kufanya .

No comments:

Post a comment