Veronica Simba – Dar es Salaam

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kushirikisha sekta binafsi katika usambazaji wa gesi asilia nchini ili kuongeza kasi yake, hivyo kuinufaisha jamii ipasavyo.

Hayo yalibainishwa jana, Machi 14, 2020 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula wakati akifanya majumuisho baada ya Wajumbe wa Kamati husika kutembelea baadhi ya makazi ya wananchi wa Dar es Salaam, waliounganishiwa gesi asilia kwa matumizi ya kupikia.

Alisema kuwa imani, matarajio na matumaini ya Wabunge ni kuona kasi ya upelekaji wa gesi asilia kwa matumizi ya wananchi, inaongezeka.

“Angalieni mbinu zitakazosaidia kuishirikisha sekta binafsi kwenye usambazaji wa gesi asilia ili twende kwa haraka zaidi.”

Aidha, Kitandula aliitaka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuwasiliana na Mamlaka zinazohusika na Mipango-Miji ili kuweka mkakati wa pamoja utakaohakikisha miji inapangwa kwa namna ambayo itawezesha miundombinu ya gesi asilia kufikishwa katika makazi ya watu na biashara kwa urahisi.

Akitoa mrejesho wa Serikali kuhusu ushirikishwaji sekta binafsi katika usambazaji gesi asilia, Kamishna na Petroli na Gesi, Adam Zuberi aliiambia Kamati kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na tayari upo Mpango - Hamasishi wa usambazaji gesi hiyo nchini.

“Tunafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wenzetu wa Shirika la Maendeleo la Japani (JICA) na tuko katika hatua nzuri,” alieleza Kamishna.

Akifafanua zaidi alisema kuwa, lengo la Mpango huo ni uwezekano wa kutumia teknolojia nafuu ya kusambaza gesi asilia nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutekeleza Mpango Kabambe wa matumizi ya gesi asilia nchini.

Zuberi alieleza malengo mengine ya baadaye kwa Mpango husika ni kuwa na mitambo midogo ya kusindika na kuchenjua gesi asilia itakayowezesha kuisafirisha kwa njia mbalimbali yakiwemo magari, badala ya kutegemea usambazaji kwa njia ya bomba peke yake.

Katika hatua za awali za utekelezaji, alisema kuwa Oktoba mwaka jana, Serikali ilipeleka timu ya wataalamu Japani kujifunza namna nchi hiyo ilivyofanikiwa katika usafirishaji gesi na kwamba Februari mwaka huu, kilifanyika kikao cha wadau jijini Dar es Salaam kueleza hatua ya utekelezaji iliyofikiwa katika Mpango huo.

Awali, akiwasilisha taarifa ya usambazaji gesi asilia nchini kwa Kamati, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio alisema ili kuongeza kasi ya usambazaji, Serikali imepanga kuendeleza miundombinu ya usafirishaji wake kwa kushirikisha kampuni binafsi katika kujenga miundombinu ya kujaza gesi katika magari pamoja na kuendeleza biashara hiyo.

Alisema kuwa, katika kutekeleza hilo, Julai 2019, TPDC ilitoa tangazo la fursa kwa kampuni binafsi kuweza kuuza gesi kwa rejareja kwa watumiaji wa nishati hiyo katika magari nchini kama ilivyo katika vituo vya mafuta.

“Kampuni 24 zimeonesha nia ya uwekezaji katika biashara ya rejareja ya ujazaji gesi kwenye magari. Kwa sasa, taratibu za kutoa leseni na vibali kwa kampuni hizo zinaendelea,” alisema.

Katika taarifa yake, Dkt Mataragio alieleza kuwa hadi kufikia Februari 2020, TPDC imejenga miundombinu wezeshi yenye urefu wa kilomita 10.8 yenye uwezo wa kuunganisha nyumba zaidi ya 10,000.

Aidha, alieleza kuwa, hadi kufikia Februari mwaka huu, jumla ya nyumba 385 na migahawa minne ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zimeunganishiwa gesi asilia huku lengo likiwa ni kufikia nyumba za awali zipatazo 1,385 jijini Dar es Salaam ifikapo Juni, 2021.

Miradi hiyo ya kusambaza gesi asilia kwa sasa inatekelezwa katika maeneo ambayo tayari kuna miundombinu wezeshi yakihusisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula (katikati), akizungumza wakati wa majumuisho baada ya Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea baadhi ya makazi yaliyounganishiwa gesi asilia kwa matumizi ya kupikia jijini Dar es Salaam, Machi 14 mwaka huu.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula (katikati) na baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo, wakizungumza na mmoja wa wakazi waliounganishiwa mtandao wa gesi asilia kwa matumizi ya kupikia (kulia), maeneo ya Mwenge Mlalakua, jijini Dar es Salaam, Machi 14, 2020.
 Kutoka kushoto ni Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Edward Ishengoma, wakiwa wameongozana na Wajumbe wa Kamati husika, kutembelea baadhi ya makazi yaliyounganishiwa mtandao wa gesi asilia kwa matumizi ya kupikia jijini Dar es Salaam, Machi 14, 2020.
 Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi akizungumza wakati wa majumuisho baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kutembelea baadhi ya makazi yaliyounganishiwa mtandao wa gesi asilia kwa matumizi ya kupikia jijini Dar es Salaam, Machi 14, 2020.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt James Mataragio akizungumza, wakati wa majumuisho baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kutembelea baadhi ya makazi yaliyounganishiwa mtandao wa gesi asilia kwa matumizi ya kupikia jijini Dar es Salaam, Machi 14, 2020.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwasili katika moja ya nyumba zilizounganishiwa mtandao wa gesi asilia kwa matumizi ya kupikia, eneo la Mwenge Mlalakua jijini Dar es Salaam, Machi 14 mwaka huu ili kujionea utendaji kazi wake.
Share To:

Post A Comment: