Wednesday, 12 February 2020

WAFUGAJI WA SAMAKI RUVUMA WATAKIWA KUONGEZA KASI


Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma ,akizungumza na Wafugaji wa Samaki wa mkoa huo.

Wafugaji wa Samaki wakimsikiliza Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma

.................................................................
WAKAZI wa Mkoa wa Ruvuma ambao hujishughulisha na ufugaji wa Samaki wametakiwa kuongeza jitihada za ufugaji huo ili kukidhi soko la walaji ambao wamekuwa wakiagiza kitoweyo hicho nje ya mkoa.mwandishi wetu Amon Mtega anaripoti toka Songea

  Wito huo umetolewa  na kaimu katibu tawala wa mkoa huo ,Jeremiah Sendoro wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya namna uandaaji  bora wa vyakula vya Samaki kwa wakazi wa mkoa huo.

   Kaimu katibu tawala huyo amesema kuwa wafugaji waliyowengi wamekuwa wakiwafuga samaki hao kiholela bila kufuata misingi bora jambo ambalo limekuwa halileti ufanisi wa ongezeko la samaki na kuwafanya wakazi wa mkoa huo kukosa kitoweyo hicho.

  Sendoro amefafanua kuwa katika sekta ya uvuvi mkoa unategemea ziwa Nyasa ,Mito na mabwawa ya kufugia samaki na kuwa vyanzo hivyo havitoshelezi mahitaji ya walaji ambayo ni zaidi ya tani 18,000 kwa mwaka jambo ambalo linafanya kupata samaki nje ya mkoa wastani wa tani 55 kwa mwezi huku uzalishaji wa samaki wa kufuga ni tani 120 kwa mwaka.

    Ameeleza kuwa kwa sasa mkoa una wafugaji wa samaki 1,513 wenye jumla ya mabwawa 1,885 yenye wastani wa uzalishaji wa tani 120.4 kwa mwaka ambao hautoshelezi kulingana na idadi ya wakazi wa mkoa huo.

    Aidha amewataka watalaamu kuendelea kuhamasisha wakazi wa mkoa huo kuongeza idadi ya wafugaji kwa kuwa tayari serikali inakituo cha kuzalisha mbegu bora za samaki katika kituo kilichopo Luhila  .

   Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka katika kituo cha utafiti wa samaki kilichopo  jijini Dar es Salaam  Dk.Gloria Yona alisema kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo kutokana na wafugaji wengi wamekuwa wakifuga bila kuzingatia kanuni hasa ya namna kuwahudumia samaki hao kwa vyakula.

 Dk.Yona amesema kuwa mafunzo hayo ya vyakula yatawasaidia wafugaji hao kuwapunguzia garama za ununuzi wa vyakula kutokana na vyakula vingi vitakavyotumika ni vinavyotokana na mazao yanayolimwa na wananchi hao,kama Soya,majani ya magimbi,pamoja na wadudu kama mchwa na kadhalika.

   Kwa upande wake mmoja wa watalaamu wa utafiti wa wadudu kwaajili ya chakula cha Samaki Gislaria Mhagama alisema kuwa kwa sasa wanatarajia kuzalisha wadudu wengi kisha kuwauzia wafugaji wa samaki ili kufanya samaki hao wawe na viwango vya ubora.

                                     

No comments:

Post a comment