Monday, 17 February 2020

Unataka Liverpool Ipi? Ya Shankly, Dalglish, Au Klopp?ROHO za ki-Merseyside. Ngoja nikupe simulizi flani kuhusu wachezaji wa Liverpool na namna ambavyo tunaipenda Timu yetu.

Unaifahamu Blackburn Rovers? Achana na hii inayopambana huko madaraja ya chini. Wala siyo ile ya muuza sura Santa Cruz.

Ipo ile Rovers ya akina Chris Sutton na Alan Sheerer. Sheerer huyu ambaye ni mfungaji bora wa muda wote England na Gwiji la Newcastle.

Unadhani aliyewapa ubingwa Rovers ni Sutton na Sheerer? Unajidanganya. Walipewa ubingwa na mwana-Liverpool.

Sir King Kenny Dalglish. Mfalme na Kocha wa mwisho kuipa Liverpool ubingwa. Ndio aliipa pia Rovers ubingwa wao wa mwisho wa Ligi Kuu.

Stori ya kusisimua ni kwamba baada Rovers kutwaa ubingwa msimu wa 1994/95 ndipo Sir Dalglish alipofanya maamuzi ya ‘ajabu’.

King Kenny alitangaza kujiuzulu ukocha wa Rovers baada ya kutwaa kombe. Na baada ya kujiuzulu ndipo alipofichua dhambi kubwa aliyowahi kuifanya maishani mwake.

Alifichua kuwa hakuna dhambi kubwa amewahi kuifanya kama kuiongoza Rovers kutwaa ubingwa huku Liverpool ikitoka patupu.

Wakati wengine wangesheherekea kwa kuweka rekodi yeye King Kenny aliona bado ni dhambi kubwa kuipa timu nyingine ubingwa.

Jezi namba saba iliyowahi kuvaliwa na Dalglish inatajwa kuwa miongoni mwa jezi zenye thamani na heshima zaidi Anfield.

Unayakumbuka maafa ya Hillsborough yale yaliyoua mashabiki wetu 96 na kujeruhi wengine 700? Basi Kocha alikua ni Dalglish. Mzee kapitia mengi huyu!

Unataka Liverpool ipi? Oke kuna ile ya ‘mungu’ wetu, Bill Shankly. Yule ambaye alianzisha spirit ya upambanaji pale Merseyside.

Ni yeye ambaye aliagiza wimbo wa You'll Never Walk Alone uwe wimbo rasmi wa klabu. Ni yeye ambaye alikianzisha kibao cha ‘This Is Anfield’

Kwaa ambao hawajui ni lazima kila mchezaji na benchi la ufundi kukigusa kibao hiko kabla hawajaingia uwanjani.

Bill alifanya hivyo ili kuwakumbusha wachezaji thamani ya kucheza Liverpool.

Ni yeye ambaye alisema duniani kuna timu bora na kubwa mbili tu. Liverpool na Liverpool ‘Reserve’

Nakupa nyingine: Bill alikua akiichukia dhahiri Everton. Huyu Mzee alikua hasimu kweli wa wale watoto wa Blue.

Aliwahi kusema “ Nikiwa sina kazi yoyote hukaa bustani kwangu na kuiangalia Everton wanavyopambana mwishoni mwa msimamo wa Ligi kuepuka kushuka daraja”

Hii ni kauli yenye kuonesha chuki ya dhahiri kwa mahasimu wetu. Na ni wazi hata Mimi naeandika makala hii siipendi haswa Everton.

Naipenda Liverpool ya Mzee Gerrard Houllier. Hii ilijawa na vijana wenye roho ya upambanaji na vipaji maridhawa kabisa.

Naachaje kumpenda Houllier ilihali yeye ndio alimpa nafasi nahodha bora wa muda wote, Steven Gerrard?

Ni yeye anaeshikilia rekodi ya mataji matatu ndani ya msimu mmoja pale Anfield. Wakati Alex Ferguson akishinda na United makombe matatu 1999, Houllier alifanya hvyo kwetu 2001.

Akiwa na Gerrard, Owen, Steve MacMaman, Jamie Redgnapp na wakali wengine aliwaongoza kushinda mataji matatu. Europa League, FA Cup na Carling Cup (Kombe la Ligi).

Sikiza wewe. Kuna Liverpool ya Rafael Benitez. Hii inatajwa kuwa Liverpool ya kibabe toka karne ya 21 iingie.

Wanaume haswa ambao wangepambana na wewe kwa dakika 90 bila kuchoka.

Usijifanye hujui tulichomfanya AC Milan 2005 na baadaye West Ham mwaka 2006. Hii ni Liverpool ya maajabu kabisa kuwahi kutokea.

Ndio Liverpool ya mwisho kumchapa Manchester United goli nne kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Achana na hiyo ya Benitez: Naipenda Liverpool ya Steven Gerrard pia. Huyu nae mapenzi yake kwetu hayapo mbali na ya Sir Kenny Dalglish.

Akiwa katika kilele chake cha ubora duniani, Real Madrid na Chelsea yake Jose Mourinho ziliweka mezani pauni 30 milioni mwaka 2004 ili kumnasa.

Kwa kipindi hicho ilikua ni pesa kubwa sana. Pengine Gerro angeweka rekodi England. Pesa kitu gani bwana? Gerro akatangaza kwamba hatoondoka na atafia kwetu.

Nini unajua kuhusu mwanaume huyu wa shoka? Ngoja nikupe mastori yake kadhaa. Usichoke!

Kwanza pamoja na kuwa na jezi zaidi ya 100 za timu tofauti kutokana na kubadilishana na wenzake lakini hana hata moja ya Manchester United.

Huwezi kuwa Kop halisi halafu ukawa na jezi za ‘Manyumbu’.

Unakumbuka fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Milan 2005? Hadi mapumziko tulikua nyuma kwa goli tatu.

Wakati wa mapumziko, Gerrard aliwatoa nje watu wote wakiwemo viongozi na benchi la ufundi kisha akabaki na wachezaji tu. Alichowaambia kinabaki kuwa siri yao. Tulivyorudi tulichomoa zote na ubingwa tukabeba.

Naipenda pia Liverpool ya Brendan Rodgers napenda namna ambavyo ilitusisimua na soka lake mujarabu licha ya kwamba tulishindwa kubeba ubingwa.

Hii ni miongoni mwa Liverpool zilizokua zikiutwanga mpira Mkubwa na wenye kuburudisha.

Kombinesheni ya Sturridge na Suarez (SAS) ilikua ni kamambe sana. Tulitoa dozi nene na soka la kuvutia.

Ni kama Rodgers aliihamishia Tik Tak ya Barcelona pale Anfield.

Mimi ni nani niache kuihusudu hii Liverpool ya Jurgen Klopp? Bwana wee. Hii ni Liverpool inayotisha ndani na nje ya uwanja.

Chini ya Klopp tumeweza kuondoka kwenye falsafa yetu ya kizamani ya kununua wachezaji wa bei nafuu na kuanza kuvunja benki.

Kama hufahamu chini ya Klopp tumeweka rekodi mbili za usajili.

Tulimsajili Virgil Van Djik kwa dau la pauni million 75 na kumfanya kuwa beki ghali duniani.

Miezi kadhaa mbele tukalipa pauni 60M tena kumnasa Allison Becker na kumfanya kuwa golikipa ghali.

Ni Klopp huyu ambaye amewavutia nyota kibao kutua Anfield. Unadhani bila yeye leo tungemmiliki Keita, Fabinho na Salah?

Unadhani bila yeye tungefika fainali tatu ndani ya misimu mitatu? Huyu Mzee amerudisha ule ubabe wetu wa enzi ya Shankly na Paisley.

Klopp huyu huyu ndani ya miezi miezi sita katwaa mataji matatu makubwa duniani. UEFA Champions League, UEFA Super Cup na World Club.

Na sasa yupo kileleni mwa msimamo wa Ligi akiongoza kwa tofauti ya alama 25 dhidi ya anaetufatia huku akihitaji pointi 15 tu kutangaza ubingwa. Yaani michezo mitano.

Ni wazi hakuna timu isiyotuogopa kwa sasa. Hao Athletico Madrid wanapiga hesabu jinsi ya kukabiliana na wale Mbwa Mwitu wetu wa Anfield.

Ghafla nimeikumbuka Liverpool ya Bob Paisley kocha ambaye ametwaa mataji mengi zaidi kuliko mwingine yeyote pale Anfield. Mataji 20 ya mashindano yote.

Paisley anatajwa kuwa Kocha wa Kiingereza mwenye mafanikio kwenye michuano ya Ulaya. Yeye, Zidane na Ancellot wanashikilia rekodi ya kutwaa mataji matatu ya Ulaya.

Ndio kocha ambaye wachezaji wake walipokua wakiumia ndani ya uwanja aliingia na kuwabeba mgongoni. Juzi juzi tumezindua sanamu lake pale Anfield.

Sitaki kuikumbuka Liverpool ya Roy Hodgson. Hii ndio Liverpool ya hovyo kuwahi kuishuhudia maishani mwangu. ‘Am sorry Roy’

Tel : 0683 015145

 Kocha wa sasa wa Liverpool, Jurgen Klopp ambaye amefanikiwa kuiongoza Timu hiyo kushinda mataji matatu ya UEFA Champions League, UEFA Super Cup na Kombe la Dunia kwa Klabu ndani ya kipindi cha miezi sita.
 Bill Shankly ambaye anatajwa kuwa kocha bora wa muda wote Katika Klabu ya Liverpool, ndiyo mwanzilishi wa falsafa na vitu vingine vingine ambavyo vimekua kama utambulisho wanaoutumia hadi leo.
 Sir Kenny Dalglish huyu ndiyo kocha wa mwisho kuipa Liverpool taji la Ligi msimu wa mwaka 1989/90. Baadaye alirejea na kuipa ubingwa Liverpool wa Kombe la Carling Cup mwaka 2002. Kwa sasa ni Balozi wa Timu hiyo.

No comments:

Post a comment