Na John Walter-Babati
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kimethodist Tanzania (TMC) , Joseph Bundala  amesema kuwa Maaskofu wote wanapaswa kutumikia nafasi zao kwa Waamini wa maeneo yote bila kujali sehemu anakotoka au alikozaliwa.

Askofu Bundala amesema hayo  katika ibada maalum ya kuwekwa wakfu kwa Askofu mpya wa kanisa la Methodist  (TMC) Jimbo la Manyara, Samuel Nyanza  iliyofanyika katika viwanja vya Kwaraa jimboni huko.

Amesema kuwa, Kiongozi yoyote wa Kanisa anafanya kazi ya kuitangaza injili ya KRISTO Pamoja na kuhakikisha amani ya nchi inazidi kulindwa.

Aidha Askofu Bundala amemwagiza Askofu  huyo mpya wa Jimbo la Manyara Samuel Nyanza, kuhakikisha anafanya kazi kwa uaminifu ambao hautakuwa na ukinzani wowote wa sheria za nchi pamoja na sheria za kanisa na isiyokuwa na machukizo mbele za Mungu.

Askofu Bundala aliwataka watumishi  wa kanisa la Methodist mkoa wa Manyara  kufanya kazi zao za kiroho na kijamii kwa ushirikiano ili kuliletea kanisa na serikali mafanikio ya kiroho na  maendeleo ya kiuchumi.

 Aidha, alimtaka Askofu mteule Samuel Nyanza  kushirikiana na serikali katika kuhakikisha nchi inasonga mbele katika kufanya maendeleo kwa faida ya wana Manyara.

Naye Askofu Mpya Samuel Nyanza amemuomba Mwenyezi Mungu amsaidie katika kutimiza wajibu wake mpya wa Kiroho katika kuwahudumia Waamini wa jimbo la Manyara, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha huduma mbalimbali za kijamii.

Ibada maalum ya kusimikwa kwa Askofu wa kanisa la Methodist (T.M.C) Samuel Nyanza wa jimbo la Manyara februari 22,2020 ilifanyika katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Maaskofu mbalimbali wa kanisa hilo na mkuu wa wilaya ya Babati Bi Elizabeth Kitundu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: