Na John Walter-Manyara

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, limeiomba serikali kurudisha huduma maeneo yote yalioharibiwa na Mafuriko kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Baraza hilo pia limeshauri kuundwa kwa kamati za Maafa kwenye kata na vijiji ili kusaidiana yanapotokea majanga kama hayo.

Kwa upande mwingine baraza limewataka wananchi kwa kushirikiana na madiwani kwenye maeneo yao kutumia nguvu zao ili kuweza kurekebisha maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.

Akifungua kikao cha Madiwani Leo Jumatano Januari 5,2020, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Nicodemus Tarmo na Diwani wa kata ya Mamire, amesema maeneo mengi ya Halmashauri ya wilaya ya Babati yameharibiwa na mvua kwa kiasi kikubwa yakiwemo mazao shambani.

 Aidha Mheshimiwa Tarmo amesema licha ya uharibifu uliotokea lakini wananchi kwa sasa wanapata adha ya usafiri baada ya baadhi ya matajiri  wenye vyombo vya usafiri kuzuia magari yao kufanya kazi wakihofia kuharibika kutokana na mvua hizo kuharibu bara bara.

Kikao hicho cha Madiwani katika kata 25 za Halmashauri ya wilaya ya Babati cha kujadili mafanikio na changamoto mbalimbali, kimefanyika  kwa mara ya kwanza kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo tangu ihamishie makao yake makuu eneo la Amref Dareda Mission kutoka Mjini Babati zilipokuwa ofisi zao awali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: