Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Patrick Kasango akiwa na timu yake kwenye moja ya mikutano ya kuhamasisha jamii kuachana na mila potofu ya Ukeketaji
Baadhi ya vitandea kazi vinavyotumiwa katika uwekezaji 

  • Na Abby Nkungu, Singida.

    BAADHI ya wazazi na walezi wa kike mkoani Singida wametajwa kuwa kikwazo katika utekelezaji wa dhana ya usalama na ulinzi wa mtoto kutokana na kubuni mbinu mpya ya ukeketaji watoto wachanga kwa siri ili kukwepa mkono wa Sheria.

    Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa baada ya Serikali  kutunga sheria inayotaja ukeketaji kuwa kosa la jinai, baadhi ya wazazi  na walezi wa kike wamekuja na mbinu mpya ambapo hutekeleza kitendo hicho kiovu na cha kikatili kwa siri usiku wa manane kwa kumsugua mtoto mchanga sehemu zake za siri kwa majivu au chumvi aina ya magadi hadi damu zitoke au kukata kwa kucha sehemu hiyo katika kutekeleza mila hiyo potofu.


    "Baadhi ya Mashirika yanajinasibu kumaliza ukeketaji kutokana na juhudi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya madhara ya mila hiyo kiafya. Ukweli ni kwamba jamii haijaacha bali kilichobadilika ni mbinu ili kukwepa mkono wa sheria" alisema  Rhoda Mtinda mkazi wa kijiji cha Makiungu halmashauri ya Wilaya ya  Ikungi ambaye anadai kuwa na taarifa za uhakika kutokana na kushirikishwa kwenye mazungumzo.

    Luth Nyampinda wa kijiji cha Siuyu Wilayani  humo  anaunga mkono taarifa hizo za siri na kuongeza kuwa licha ya madhara ya kiafya yanayotajwa na Wataalamu na kukiuka misingi ya haki za binadamu, bado sio rahisi kwa jamii kuacha kabisa ukeketaji kutokana na kugusa imani zao za kimila. 

    "Baadhi ya wananchi wameingiwa na mila hii hadi kwenye mishipa ya damu hivyo sio rahisi kuiacha kabisa kwa haraka.  Ni suala la muda, tena muda mrefu" alisema Luth na kuongeza kuwa baadhi ya wenyeji wanaamini, pamoja na mambo mengine, kuwa ukeketaji unatibu ugonjwa ujulikanao kama "lawalawa".

    Kutokana na hali hiyo, wengi wa wananchi wanasema kuwa bado ukeketaji unaendelea kufanyika; hasa kwa watoto wachanga, safari hii akinamama ambao wanapaswa kumlinda na kuangalia usalama wa mtoto, wakitajwa kuwa vinara wa kukiuka ulinzi na usalama wa mtoto, kwa kisingizio cha kutii kiu ya imani za kimila wakidai ni  tiba kwa magonjwa, huondoa mikosi katika familia na kuleta heshima kwa jamii inayowazunguka. 

    Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya Wanawake na Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida,  Dk Suleiman Muttani alipohojiwa alithibitisha kuwa ni kweli ukeketaji kwa watoto wachanga sasa hivi ndio umeshika kasi.

    "Kutokana na vichanga hao kuletwa hospitalini na kwenye Vituo vya kutolea huduma ya afya kwa ajili ya kupatiwa huduma mbalimbali za mtoto, tumebaini jambo hilo ovu na la kikatili wakati wa  utendaji wetu wa kazi" alieleza Dk Muttani.

     Aidha, alikanusha kuwepo ugonjwa wa "lawalawa" kwa watoto, wasichana wala wanawake na kusema kuwa kinachofanyika ni kisingizio tu ili kutekeleza mila hiyo potofu..

    Alisema kuwa mila hiyo ya ukeketaji ni kikwazo  cha utekelezaji wa  dhana ya ulinzi na usalama wa mtoto mkoani Singida kutokana na athari za kiafya na kisaikosojia kwa watoto husika ikiwa ni pamoja na athari za  muda mrefu na muda mfupi.

    "Athari hizo ni kutokwa na damu nyingi sehemu za siri au wakati mwingine husababisha kifo na maambukizi ya magonjwa ya Ukimwi. Magonjwa ya kuambukiza ya mara kwa mara yanayoweza kumfanya mtoto kuwa tasa anapofikia ukubwani, uharibifu wa mfumo wa njia ya uzazi, matatizo wakati wa kujifungua na kutofurahia tendo la ndoa wakati wa kujamiana kutokana na kovu linalobaki baada ya majeraha kupona" alifafanua Dk Muttani.

    Takwimu za utafiti wa Kidemografia na Afya (TDHS) zinaonesha kiwango cha ukeketaji wanawake wenye umri wa miaka 15 - 49 kimekupungua kutoka asilimia 18 mwaka 1996 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2015/16.

    Ingawa Kitaifa hali ya ukeketaji inaonesha kupungua, Dk Muttani anasema takwimu za idara ya afya mkoani Singida zinaonesha wastani wa asilimia 23 ya wanawake wanaokwenda kujifungulia kwenye vituo vya huduma za afya wanagundulika kuwa wamekeketwa; baadhi yao wakiwa bado wachanga na bila ridhaa yao. 

Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: