Saturday, 4 January 2020

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YAKUTANA NA WADAU WA UCHAGUZI MIKOA YA LINDI NA MTWARA

Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Asina Omar akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwenye Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi uliofanyika Mkoani Mtwara 

Bw. Musa Kulangwa kiongozi wa chama cha CUF akichangia hoja kwenye Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi

……………..

Mtwara,

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewahimiza wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Wakizungumza kwenye mikutano ya wadau wa Uchaguzi iliyofanyika leo (Ijumaa tarehe 03.01.2020) mkoani Lindi na Mtwara ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mst.) Mbarouk Salim Mbarouk na Mjumbe wa Tume, Mhe. Asina Omar wamesema zoezi hilo kwa Lindi na Mtwara litafanyika kwa siku saba (7) kuanzia tarehe 12 hadi 18 mwenzi huu.

Wadau walioshiriki mikutano hiyo ni pamoja na Viogozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wawakilishi wa makundi maalum ya Watu wenye Ulemavu, Vijana, Wanawake na Wazee.

Wakisoma hotuba za ufunguzi wa mikutano hiyo, viongozi hao wamesema kwamba “kabla ya kuanza kwa awamu ya kwanza (ya Uboreshaji wa Daftari), Tume ilifanya maandalizi kadhaa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa Vituo vya kujiandikishia, Uandikishaji wa majaribio, Maandalizi ya vifaa vya Uboreshaji wa Daftari pamoja na kuandaa Mkakati wa Elimu ya Mpiga Kura”.

Tangu kuzinduliwa kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mnamo tarehe 18 Julai, 2019 mkoani Kilimanjaro, tayari mikoa kumi na nane (18) imekamilisha zoezi hili. Mikoa hiyo ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara, Mwanza, Kigoma, Tabora, Songwe, Kagera, Geita, Shinyanga, Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Mbeya na Iringa. Zoezi hilo hivi sasa linaendelea katika mikoa ya Ruvuma na Njombe kwa Tanzania Bara na Visiwa vya Unguja na Pemba kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Akitoa mada kwenye mkutano mkoani Mtwara, Mkurugenzi waUchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles ametoa wito kwa Wadau hao kutoa ushirikiano katika kuelimisha, kuhamasisha na kufuatilia zoezi hili. Aidha, amewataka kufanikisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili wale wote wenye sifa waweze kuandikishwa au kurekebisha taarifa zao katika Daftari.

No comments:

Post a comment