Saturday, 4 January 2020

DKT. BASHIRU AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUWAANDAA WANANCHI KUPOKEA MABADILIKO
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally, leo ameungana na waumini wengine wa dini ya Kiislamu kushiriki Ibada ya Ijumaa katika msikiti wa Mkoa uliyopo Manispaa ya Bukoba, ambapo amewaomba viongozi wa dini zote nchini kuwaandaa wananchi kupokea mabadiliko ya kimaendeleo katika nchi yetu.

Katika ibada hiyo, Katibu Mkuu akitoa salam za Ijumaa, ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini kuwaandaa wananchi kupokea mabadiliko yanayoendelea kutokea nchini, kutambua na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na mabadiliko hayo.

“Viongozi wa dini tunawaomba mtutayarishe wananchi kushiriki, kutambua na kutumia fursa za mabadiliko ya maendeleo nchini, kuna miradi mikubwa inatekelezwa, ikiwemo ujenzi wa miradi ya kimkakati ambayo hapo awali haikuwepo, mathalani, mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa, mradi mkubwa wa umeme Rufiji, ujenzi wa vivuko vikubwa kama cha Busisi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, uanzishwaji wa hifadhi mpya kama Burigi na miradi mingine mingi.”

Akisisitiza hilo ameongeza kuwa, viongozi wa dini ni vema kuendelea kuwaandaa wananchi kutumia fursa hizo kwa maisha yetu, mathalani uanzishwaji wa hifadhi ya Burigi itatoa fursa kwa watalii wengi maeneo ya Kanda ya ziwa, sasa ni vema wananchi wakaanza kuelewa fursa zilizopo sambamba na uwepo watalii katika maeneo yao.

Aidha, Katibu Mkuu, ameendelea kuwaomba viongozi wa dini kote nchini, kuhamasisha umoja, mshikamano na kuendelea kuliombea Taifa hasa tunapoelekea kipindi cha uchaguzi kuwawezesha wananchi kuamua vema bila jazba, kwa kujitathmini ili kupata viongozi walio bora kwa ngazi zote.

Katika Ibada hiyo, Shekhe wa Mkoa wa Kagera Alhaji Haruna Kichwabuta akitoa mawaidha, kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, amewaomba wananchi kujenga tabia njema ya kushukuru kwa jambo lolote jema wanalotendewa, ambapo huanza ngazi ya mtu na mtu, ndani ya familia, mtu na jamii mpaka wananchi na Serikali.

’’Tujenge tabia ya kushukuru kwa kidogo tunachosaidiana, hata serikali wakifanya jambo zuri, mfano ni watoto wangapi walikuwa hawaendi shule, leo wanakwenda wote bila malipo, hapa serikali haijafanya tu wajibu ila imetenda wema na utu, vituo vya afya vimejengwa kila mahala, barabara zimeendelea kujengwa kila mahala, vivuko ndio usiseme, ila bado kuna watu wanasema serikali imefanya nini, hawa hawana shukrani.”

Katibu Mkuu yupo Bukoba Mkoani Kagera kwa mapumziko ya siku kumi ambapo anatarajiwa kumaliza mnapumziko hayo mapema mwezi Januari, 2020.

Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM

No comments:

Post a comment