Na. Catherine Sungura-Dodoma

Hospitali ya Benjamin Mkapa imetakiwa kujiunga na tiba mtandao ili kuweza kutoa tiba kwa wagonjwa  kwa haraka na kwa ufanisi ili kuwapunguzia wagonjwa muda wa kusubiri majibu hususani ya mionzi .

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati alipoitembelea hospitali hiyo kujionea hali ya utoaji huduma.

“Nawaelekeza ni vyema mkajiunga na huduma ya tiba mtandao ili muweze kutoa huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi, mnatakiwa mkajifunze huduma hii kutoka hospitali ya Muhimbili au MOI". Amesema waziri Ummy.

Aidha, Waziri huyo amesema kuwa hivi sasa kwenye hospitali nyingi kuna changamoto za wataalam wa kusoma picha kwani wataalam wengi waliopo ni wale wa kupiga ”bahati nzuri sisi tunao wataalam wengi wa kupiga picha mana kwenye mionzi kuna aina mbili za wataalam wapo wa kupiga picha (radiographer) na wa kusoma picha, hivyo serikali itahakikisha inapata wataalam wengi zaidi wa kusoma ili kukidhi mahitaji.

Waziri Ummy amesema wizara ina lengo la kuziunganisha hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya kwenye mfumo wa hospitali za rufaa za mikoa kwa kufunga senta zitakazosaidia hospitali za wilaya na vituo vya afya vinavyofanya vipimo vya ‘utra sound’ na ‘x-ray’ na majibu yakasomwa haraka na wataalam wa Hospitali za rufaa na kutoa majibu haraka bila kumsubirisha mgonjwa kwa muda mrefu.

Alitaja hospitali zilizojiunga na tiba mtandao  ni pamoja na hospitali za rufaa za mikoa ya Lindi na Morogoro , pia hospitali teule za wilaya  za Nyangao,Turiani na hospitali za wilaya  ya Nachingwea,kilosa na Mvomero.

Wakati huo huo Waziri Ummy ameitaka hospitali hiyo kupunguza gharama za kulipia uchunguzi wa saratani ya matiti kwa wanawake kutoka elfu sabini hadi elfu thelathini kama hospitali zingine za taifa zinavyofanya.

Hata hivyo waziri huyo ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani  kutosafiri hadi dar es salaam kupata huduma za kibingwa kwani huduma zote karibu zinapatikana hapo na hivyo ameahidi wizara wataleta madaktari bingwa wa mishipa ya fahamu pamoja na mifupa.

_Mwisho-
Share To:

msumbanews

Post A Comment: