Sunday, 15 December 2019

PHILA NDWANDWE NI SHUJAA ALIYEUWAWA KIKATILI.Mwaka 1960 serikali ya kikaburu ya Afrika Kusini ilifanya mauaji ya halaiki kwa raia wasio na hatia waliokua wanaandamana kupinga udhalimu wa serikali hiyo kwa watu weusi. Mauaji hayo maarufu zaidi kama 'Sharpeville massacre' yalitokea March 20, katika mji wa Sharpville, ambao leo unajulikana kama Gauteng.

Baada ya mauaji hayo chama cha ANC kiliamua kubadili mbinu ya mapambano, kwa sababu njia zote za kudai haki kwa amani zilifeli.

Njia ya mazungumzo, maandamano na migomo hazikufaa tena katika kudai haki.Serikali ya kikaburu ilizuia watu wasiseme, wasifanye mikutano ya kisiasa, wala maandamano. Hakukua na uhuru wa vyombo vya habari wala uhuru wa maoni.

 Yeyote aliyetoa maoni yasiyoifurahisha serikali aliishia gerezani ama kupotezwa.

 Walioandamana walipigwa risasi na kufa. Serikali haikujali.

Kwahiyo ANC wakaamua kubadili mbinu. Wakaunda kikundi cha kupigana msituni kiitwacho uMkhonto we Sizwe (MK), neno la kizulu lililomaanisha 'mkuki wa taifa'.Haraka sana serikali ya kikaburu ikatangaza kuwa kikundi hicho ni cha kigaidi na ikakipiga marufuku.

 Ikawakamata viongozi wa ANC akiwemo Nelson Mandela na Walter Sisulu na kuwasweka jela kwa tuhuma za kuanzisha kikundi cha kigaidi.

 Walikamatwa usiku wa tarehe 11 July, mwaka 1961 huko Rivonia, shambani kwa Muisrael mmoja aitwaye Arthur Goldreich aliyekua akiwafadhili ANC kwa siri. Goldreich nae 'alisukumwa ndani' pamoja na kina Mandela.

Baada ya kukamatwa Mandela aliwaambia wafuasi wake wasikate tamaa, waendelee na mapambano.

Alitumia maneno ya kizulu 'Ngethemba ngoba kusasa' ambayo tafsiri yake kwa Kiswahili alimaanisha 'kesho kuna matumaini zaidi kuliko juzi au jana. Kwa lugha rahisi ni sawa na kusema 'KESHO NI NZURI KULIKO JANA'Kikundi cha MK kiliendeleza mapigano dhidi ya serikali dhalimu ya makaburu.

Mapigano hayo yalichukua muda mrefu sana. Wakati Mandela akisota gerezani, kikundi hicho chini ya uongozi wa Muzi Ngwenya kiliendeleza mapambano kikiweka ngome yake huko Swaziland.'Kili-recruit' na 'kutrain' vijana kwa ajili ya mapambano.

 Mmojawapo ni mwanadada Phila Ndwandwe aliyejiunga na MK mwaka 1985.

 Alikua miongoni mwa wanawake wachache waliokua wapiganaji katika kikundi hicho.

 Alishiriki kupigana vita vya msituni kuondoa utawala dhalimu wa kikaburu. Aliamini jukumu la ukombozi halikua la wanaume peke yao, bali la kila mtu.Bahati mbaya mwaka 1988 Phila alikamatwa na askari wa kikaburu akiwa anamnyonyesha mwanae huko msituni. Alipigwa na kuteswa sana akilazimishwa atoe siri za kikundi cha MK lakini aligoma.

Kabla ya kukamatwa Phila alikua askari shupavu ambaye licha ya kuwa na mtoto mchanga hakuacha kupigana.

Alishika bunduki mkono mmoja huku mkono mwingine ukinyonyesha.Baada ya kumshikilia mateka kwa siku kadhaa, serikali ya kikaburu ilitangaza kuwa ilimwachia huru na kwamba eti alikimbilia Tanzania.

Kwahiyo familia ya Phila iliamini binti yao yupo Tanzania, lakini ukweli ni kuwa alikua katika mateso makali sana akipigania uhai wake na mwanae huko Swaziland.

Askari katili wa kikaburu waliamuru mbwa wamuume, kisha wakamvua nguo zote na kumtandika mijeledi sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mmoja wa askari aliyemtesa Phila alikuja kukiri na kuomba msamaha mwaka 1994, kwenye Tume ya Ukweli na Maridhiano baada ya utawala wa kikaburu kuangushwa. Askari huyo alisema kuwa walimuweka Phila katika chumba cha mateso akiwa uchi wa mnyama kwa siku 10.

 Siku ya 6 ilimbidi Phila ajitengezee nguo ya ndani kwa kutumia mifuko ya plastiki iliyokua imezagaa kwenye chumba hicho.Walimuwekea makaa ya moto na kumlazimisha akanyage, na kuna wakati walimtoboa na misumari sehemu mbalimbali za mwili wake.

Baadae walimtoboa macho, na hivyo kushindwa kuona. Hata hivyo hakutoa siri za kikundi cha MK, licha ya mateso yote hayo.

Baada ya siku 10 za mateso makali walimkata maziwa ili asiweze tena kumnyonyesha mwanae.

Kisha wakamfunga mikono na miguu na kumpiga risasi kichwani yeye na mwanae na kuwazika kwenye kaburi la pamoja.

Baada ya Afrika Kusini kupata uhuru mwaka 1994, serkali ya ANC (black majority) iliandaa kumbukumbu ya mashujaa wake.

Mmojawapo ni Phila Ndwandwe, mwanamke shupavu ambaye damu yake ilimwagilia ukombozi wa taifa hilo. Rais Nelson Mandela aliagiza mabaki ya mwili wa Phila yafukuliwe huko Swaziland, na kuletwa Afrika Kusini yazikwe kwa heshima.

Tarehe 12 mwezi March, mwaka 1997 taifa zima la Afrika kusini liliungana katika ibada ya kuzika upya mabaki ya mwili wa Phila huko KwaZulu Natal, kwenye shamba la Elandkop walikozikwa mashujaa wengine.

No comments:

Post a comment