Na.Catherine Sungura

Kituo cha afya Kome kilichopo halmashauri ya buchosa wilayani Sengerema kimefanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza  wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni na hivyo kumuokoa mama na mtoto wake.

Akiandika kwenye mtandao wa kijamii Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa kwa mara ya kwanza kituo hicho kimeweza kufanya upasuaji huo baada ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  kujenga “theatre” na kuweka vifaa tiba kwenye kituo hicho.

Waziri Ummy ameendelea kuandika kuwa chumba hicho cha upasuaji ambacho kipo kituoni hapo kitawasaidia akina mama wajawazito wa kisiwa cha kome watakaopata uzazi pingamizi na hivyo kutokufuata huduma hizo wilayani sengerema na hivyo kutokuvuka tena maji.

“Hakika tumedhamiria kuokoa maisha  ya akina mama wajawazito na watoto wachanga,tutaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha huduma za uzazi  za dharura ikiwemo ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni(CEmONC) zinapatikana katika vituo vyote vya afya vya umma ,mama na mtoto huyo mwenye uzito wa kilo 3 na nusu wanaendelea vizuri”Amesema waziri Ummy

Naye Mganga Mkuu wa halmashauri ya buchosha Dkt. Ernest Chacha amesema walimpokea mama huyo kituoni hapo siku ya ijumaa ambaye alikua akihudhuria kliniki kwenye zahanati moja huko kisiwani hakuweza kujifungua kawaida kwani alikua akikabiliwa na uchungu pingamizi kwani nyonga zake  hazikuwa zinapanuka hivyo ili kumuokoa ilibidi afanyiwe upasuaji kuweza kumuokoa mama pamoja na mtoto .

Dkt. Chacha ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa uboreshaji wa vituo vya afya nchini ikiwemo kituo cha afya cha kome ambacho kipo kisiwani kwa kuboresha miundombinu kwa kujengewa chumba cha upasuaji pamoja na kuwekewa vifaa tiba hivyo kusaidia kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na watoto wachanga hususan visiwani humo.

“Wananchi walikua wanapata adha kubwa sana ya kuvuka maji kutoka kisiwani na kufuata huduma kwenye hospitali ya wilaya iliyopo sengerema,tunamshukuru Waziri Ummy Mwalimu kwa kuiagiza MSD kutufungia taa kwenye chumba cha upasuaji wakati wa ziara yake hivi karibuni visiwani hapa kwani tumeweza kuokoa maisha ya huyu mama muda mfupi baada ya taa hizo kufungwa”Amesema Dkt. chacha

Hivi karibu waziri wa afya alitembelea kisiwa hicho na kuwaahidi  kuwapatia xray mashine ya kidigitali  kwenye kituo hicho cha afya na kuwataka MSD kufunga taa kwenye chumba hicho cha upasuaji mara moja.

Kisiwa cha kome kimeongeza  idadi ya akina mama wanaojifungulia  kwenye vituo vya afya  kwa  asilimia 80  kwa mwaka ambapo wastani akina mama  50 wanajifungulia kwa mwezi
Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: