Sunday, 15 December 2019

DKT TULIA AONGEZA KASI YA TANZANIA KUNG'ARA KATIKA MICHEZO

Naibu spika wa bunge la Tanzania Dkt Tulia Ackson akiwa na bendera ya Tanzania baada ya kufanya vema kwenye  mchezo wa kutembea kwa kasi mita 1600

Wabunge wa bunge la Tanzania waliopo nchini Kenya katika michezo ya mabunge Afrika wameendelea kuibuka kidedea katika michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki baada ya Leo kuzoa dhahabu mbili kwenye mbio za mita 800  na Kutembea kwa kasi maarufu kama Walk race.

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dkt Tulia Ackson kwa mara ya tatu mfululizo ametwaa dhahabu katika mchezo wa kutembea kwa kasi mita 1600 baada ya kutembea kwa dakika 12.04 akifuatiwa na Edith Nyenze wa Bunge la Kenya dk 12.14, wakati Zaituni Diriwaru wa Uganda akimaliza wa tatu kwa 12.43.

 Anatropia Teonest ambaye juzi alimaliza nafasi ya Pili katika mita 400 na 1500, Leo ametwaa dhahabu katika mbio za mita 800 kwa dakika3. 18 wakati Yosepher Komba akatwaa Fedha baada ya kukimbia dakika 3.19 akifuatiwa na Anna Adeke wa Uganda kwa dakika 4.00.

Katika mbio za mita 200 Ester Matiko aliibuka mshindi wa pili akifuatiwa na Rose Tweve aliyetwaa nafasi ya tatu.

Michezo hiyo inaendelea nchini Kenya kwenye Uwanja wa Mandela-Nambole kwa michezo ya kuvuta Kamba na mbio za kupokezana vijiti, wanaume na wanawake.

No comments:

Post a comment