Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally leo tarehe 04 Desemba, 2019 amehitimisha ziara yake ya siku tisa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuzungumza na wazee wa Pemba.

Katibu Mkuu ameitumia fursa hiyo kusikiliza maoni ya wazee, ushauri, mapendekezo, na changamoto mbalimbali katika kuboresha zaidi huduma kwa wananchi na kufahamu ni kwa kiasi gani wazee wameridhika na mwenendo wa serikali zote mbili za Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais  Dkt. Ali Mohamed Shein na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Wazee hao wa Pemba katika mazungumzo hayo kwa kauli moja, wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ufanisi wao wa kusogeza karibu huduma za jamii pamoja na  kudumisha Muungano wakati wote.

"Sisi tunampongeza sana Rais wetu Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, kazi tuliompatia anaifanya vizuri sana na tunasema kwa  kauli moja, tunamtaka aendelee hivo, Pia tunamshukuru sana Rais wetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kudumisha umoja wetu, upendo, amani na utulivu katika kipindi hiki cha miaka tisa ya uongozi wake hakika tunafarijika sana". Mzee Hamis Ali Mzee.

Katibu Mkuu akizungumza ma wazee hao, ameeleza umuhimu wa kuwa karibu na wazee wetu ambao muda mrefu wa maisha yao wameutumia katika ujenzi wa Nchi na Taifa tulilonalo sasa.

"Viongozi wenzangu ni lazima tuwe na utaratibu wa kukutana na wazee wetu, wazee hawa wana mambo mazuri ya kujifunza kwao katika kipindi hiki ambacho bado wananguvu za kuzungumza na kufundisha ili tuzidi kupata maarifa mengi walionayo." Katibu Mkuu ameeleza

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu  amezuru  kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Dkt. Omary Ali Juma aliyefariki mwaka tarehe 04 Julai,  2001.

Dkt. Bashiru ametumia wasaa huo kueleza kwa ufupi wasifu wa hayati Dkt. Omari ambapo amesema, 

"Dkt. Omari Ali Juma alisimamia dhana ya kuishi pamoja kwa upendo, amani, kuvumiliana na kuhimiza maendeleo, nakumbuka pia alivyosimamia kwa uthabiti kampeni ya mazingira akiwa Makamu wa Rais." Ameeleza

"Ndani ya Chama Chetu, viongozi na wanachama wote waliotoa mchango wao katika kukijenga Chama tutaendelea kuwaenzi na vijana ni lazima mpangilie maisha yenu vizuri ili mtoe mchango mkubwa zaidi kwa Taifa letu." Ameongeza.

Aidha, Katibu Mkuu amewatembelea wazee na wagonjwa mbalimbali Mkoa wa Kusini Pemba wakiwemo Mzee Khalidi Ali Khalid na Mzee Ali Suleimani Makasi.

Ziara hii ya siku tisa ambayo imehitishwa leo  kisiwani Pemba imelenga katika kuimarisha Uhai wa Chama na Jumuiya zake na kuimarisha mahusiano baina ya viongozi wa Chama na Serikali pamoja na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020.

Imetolewa na;
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: