Na. Catherine Sungura, Mwanza

Serikali ya Tanzania inatenga mabilioni mengi katika kushughulikia masuala ya afya nchini hususani kwenye upande wa tiba ambapo gharama za matibabu zinakuwa kubwa sana.

Hayo yamesemwa leo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai wakati kusaini tamko la maazimio ya viongozi wa dini lililobeba ajenda ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua kikuu (TB) nchini  jijini hapa .

“Wananchi wanadhani kuwa wizara ya afya inasimamia tu tiba, hapana tusisahau kinga ni muhimu sana  dhidi ya magonjwa nchini, tutakaposimamia kinga  serikali itakua inaokoa gharama kubwa kwenye matibabu na pia kupunguza mzigo mkubwa wa kugharamia matibabu kama nchi”Alisisitiza Mhe. Ndugai

Aidha, amewashuru viongozi hao wa dini kwa ahadi pamoja na kusaini azimio  la kusimamia na kusemea kwa waumini  wao suala zima la TB hivyo anayo Imani watalibeba na kulitekeleza na kuwafanya wananchi wengi kupata uelewa juu ya ugonjwa huo na kujitokeza  mapema kwenda kupima afya zao na hivyo kuanza dawa  na  kutoambukiza watu wengine.

Awali akiongea na viongozi hao Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  amesema kuwa Wizara yake  inaendelea kubuni mikakati ya kutokomeza  Tb nchini kama  mikakati Madhubuti yaliyowekwa   kwa mara ya kwanza na baraza kuu la umoja wa mataifa lililokutana Septemba mwaka 2018 na kuweka maazimio na malengo ya  kuongeza kasi ya  kutokomeza TB  ifikapo mwaka 2030.

“Maambukizi mapya ya Tb nchini yamepungua kwa asilimia 18 kulinganisha  na hali ya mwaka 2015 na hivyo kufanya Tanzania  kuwa miongoni  mwa nchi saba  Duniani ambazo zipo katika mwelekeo sahihi wa kufikia malengo ya mpango mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kutokomeza TB kwa hatua ya kwanza ya mwaka 2020.

Aidha, Waziri Ummy amesema  kuwa vifo vitokanavyo na Tb peke yake vimepungua kutoka 30,000 mwaka 2015 hadi 22,000 mwaka 2018 na hii ni sawa na punguzo la asilimia 27,“licha ya mafanikio, nchi bado ina vifo vingi vinavyosababishwa na Tb ambapo kwa sasa takribani watu sitini  hufariki   kila siku hapa nchini”, alisema .

Hata hivyo Waziri huyo wa afya amesema kuwa hadi kufikia mwaka huu serikali ina vituo 103 vinavyotoa huduma za wagonjwa wenye Tb sugu ukilinganishwa na kituo kimoja mwaka 2015  pamoja na uboreshaji wa mifumo ya  uchunguzi  na ugunduzi wa TB kwenye vituo vya  huduma za afya,upanuzi wa matumizi ya hadumini za kisasa za LED na kuongezeka kwa mashine za kisasa zinazopima vimelea vya TB kwa njia ya vina saba za GenXpert zipatazo 238 ambazo kwa sasa zinapatikana kwenye mikoa yote nchini.
-Mwisho-
Share To:

msumbanews

Post A Comment: