WENYEVITI wa Mitaa na Wajumbe wao wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo katika kuwatumikia wananchi ili kuendana na azma ya Mhe Rais Magufuli ya kuwaletea watanzania maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Godwin Kunambi wakati akizungumza na wenyeviti wa mitaa na wajumbe baada ya zoezi la kuwaapisha kufanyika.

Kunambi amesema wananchi wana changamoto na kero nyingi ambazo zinapaswa kutatuliwa hivyo ukiwa kiongozi unapaswa kushughulika na mambo ya wananchi waliokuchagua bila kujali itikadi za vyama na Dini zao.

Amesema wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe ndio viongozi ambao wanakutana na wananchi na kugundua changamoto zao hivyo ni jambo la ajabu kuona mwananchi anaenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya au kwa Mkurugenzi ilihali mtaa una viongozi wake.

" Ndugu zangu kama anavyosemaga Mhe Rais hizi kazi za watu siyo lelemama, tumeomba wenyewe ridhaa ya kuwatumikia watanzania basi tuwatumikie kwa moyo wote na tusiweke maslahi yetu mbele.

Nafahamu kumekuepo na tabia ya wenyeviti kutaka pesa pale mwananchi anavyofika kwake kuhitaji huduma fulani, nitoe rai kwenu kuwa wazalendo na kuishi katika uongozi ambao Rais Magufuli amekua akiuishi kwa kuwa muadilifu, mchapakazi na mzalendo kwa watu wetu waliotuchagua," Amesema Kunambi.

Amewataka kwenda kufanya kazi kwa kufuata Katiba ya Nchi na miongozo ya kiutendaji ya Serikali za Mitaa lakini pia akawasihi kushirikiana na watendaji wao katika kuwaletea wananchi maendeleo na kuzifikia changamoto zao kwa wakati.

Pia amesema Jiji la Dodoma litaandaa utaratibu wa kuwafanyia semina viongozi hao ya kuwapitisha kwenye sheria, kanuni ili waweze kujua mamlaka waliyonayo.

" Tutaanzisha pia utaratibu wa kutoa zawadi nono kwa mitaa 10 bora ambayo itafanya vizuri katika nyanja mbalimbali kwenye Jiji letu, rai yangu kwenu nendeni mkafanye kazi bila kubagua na mjue wananchi wamewaamini," Amesema Kunambi.

Jumla ya wenyeviti 222 na wajumbe wa serikali za mitaa 1110 ndani ya Jiji la Dodoma wameapishwa leo baada ya uchaguzi uliofanyika Novemva 24 mwaka huu ambapo viongozi wote hao wanatokana na Chama cha Mapinduzi.
 Wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa jijini Dodoma wakila kiapo cha uongozi leo tayari kwa kuanza majukumu ya kuongoza mitaa yao kwa kipindi cha miaka mitano inayokuja.
 Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi akizungumza na wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wao katika mkutano wa pamoja baada ya kuapishwa leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi akizungumza na wenyeviti wa mitaa 222 pamoja na wajumbe 1110 waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka huu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment:

Back To Top