Katika mwendelezo wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) kwenye mikoa ya kusini, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Tanzania (DPP) Biswalo Mganga amefuta jumla ya kesi 59 katika mahakama za Mkoa wa Mbeya.

Mkurugenzi Biswalo ameyafanya hayo katika gereza la Ruanda mjini Mbeya na gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe alipoambatana na Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Mahiga ili kujionea hali halisi ya mazingira ya utoaji haki jinai katika magereza hayo na taasisi mbalimbali za haki jinai ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Polisi, Mahakama na Magereza yenyewe.

“Niliowafutia Kesi nendeni mkawe raia wema, msirudie makosa, badala yake mkawe mabalozi wema mtakaofanya kazi kwa bidii ili kumuunga mkono Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Maguli katika kauli yake ya hapa kazi tu.”

Kwa upande wake Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) aliwataka wote waliofutiwa mashitaka kwenda kufurahi na familia zao huku wakimshukuru Mungu na kujutia makosa yaliyosababisha kushitakiwa kwao. Aidha, aliwaonya kutokurudia makosa hayo badala yake watumie nguvu na akili walizonazo kuzalisha mali kwa maendeleo yao na familia zao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.

“Mliosamehewa leo nendeni mkafurahi na familia zenu sambamba na kuwa watu wema katika jamii inayowazunguka kwani ni matumaini yangu kuwa mmejifunza mengi na mmebadilika. Kuna watu hapa nikiwatizama misuli yao, walipaswa wakaitumie kufanya kazi na kuzalisha mali kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla badala ya kuitumia kufanya uhalifu.”

Kwa mujibu wa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo 2002, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka anayo mamlaka ya kuwafutia mashitaka watuhumiwa wa makosa ya jinai katika magereza mbalimbali nchini. Mpaka sasa katika ziara hii ya kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria katika mikoa mitatu DPP Biswalo ameshafuta  jumla ya kesi 120 na bado ziara inaendelea katika Wilaya ya Kyela na baadae mkoa wa Njombe.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: