Ferdinand Shayo, Arusha

Zaidi ya wananchi 6000  kutoka vijiji vinne  vilivyopo kata ya Oldonyowas  katika halmashauri ya Arusha wanatarajia kunufaika na huduma za afya na kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu huku  wanawake wakijifungulia njiani kutokana na umbali  wakati wa kufuata huduma za afya.

Aidha wananchi hao,ni kutoka vijiji vya Losinon  Engutukoit,Kisimiri juu, na Wiro ambapo  watanufaika na zahanati ya kisasa iliyojengwa na wahisani kutoka nchini Ujerumani kupitia shirika la Help for Maasai Children  (HMC).

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi na kulikabithi jengo hilo kwa halmashauri ya Arusha katika kijiji cha Losinon juu kata ya Oldonyowas, Mkurugenzi wa shirika hilo la HMC kwa Tanzania,Joseph Kivuyo alisema kuwa,ujenzi wa zahanati hiyo ulianza rasmi Juni 26,mwaka huu ambapo hadi sasa hivi mradi umekamilika kwa asilimia 85.

Kivuyo alisema kuwa, mradi wa zahanati hiyo mpaka  sasa hivi umegharimu kiasi cha shs 108 milioni na hadi kukamilika utagharimu kiasi cha shs 140 milioni ,ambapo wananchi hao wataweza kuondokana na changamoto mbalimbali za kutembea  umbali mrefu kufuata  huduma za afya .

Aliongeza kuwa, wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakitembea kilometa 8 hadi 12 kufuata huduma za afya,ambapo kutokana na umbali huo wanawake wengi wamekuwa wakijifungulia njiani na wengine majumbani na kuchangia Vifo kutokana na kutokwa na damu nyingi hali inayochangiwa  na huduma za afya kuwa mbali.

"ujenzi wa zahanati hii tumeshirikiana na serikali ya halmashauri ya Arusha ambao walitupa ramani ya zahanati hii ,ndipo wahisani wetu kutoka Ujerumani waliamua  kutujengea zahanati hii,baada ya kuja na kuona uhitaji mkubwa uliopo ikiwemo wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya na tunawashukuru sana kwani wananchi wetu wataanza kunufaika sasa."alisema Kivuyo.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru ,Jerry Muro akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi aliwapongeza wafadhili hao kwa hatua hiyo ya kusaidia miradi mbalimbali katika kata hiyo ikiwemo elimu na Afya ,ambapo alisema mfano huo unapaswa kuingwa na wadau wengine.

Aidha aliwaahidi wananchi hao kuwaletea gari aina  ya Landcruiser kwa ajili ya kubebea wagonjwa ambapo litakuwa linatoa huduma katika zahanati hiyo,huku akiwaahidi kutengeneza barabara inayoelekea  katika zahanati hiyo ili kurahisisha  huduma  kufika kwa haraka kwa wananchi hao.

Naye Mfadhili wa mradi huo ambaye ni Mkurugenzi  wa shirika hilo nchini  Ujerumani,Harald Pfeiffer  alisema kuwa, ujenzi wa zahanati hiyo ni mojawapo ya ndoto alizojiwekea muda mrefu  za kuhakikisha anasaidia jamii hiyo katika sekta ya elimu, na Afya .

Aliwataka  wananchi wa kata hiyo kutumia mradi huo kwa manufaa yaliyowekwa huku akiwataka kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na  kutumika kwa vizazi vijavyo.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho,Lightnes Gabriel na Anna John walisema kuwa,wanashukuru sana kwa mradi huo  kwani umekuja muda maufaka ambao walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa huduma za afya katika kata hiyo na uwepo wa zahanati hiyo utaweza  kuondoa changamoto kubwa ya  wanawake kujifungulia njiani na majumbani kutokana na kufuata huduma mbali.

Aidha waliiomba serikali kukamilisha na kuharakisha hatua iliyobaki ikiwemo ya  uletaji wa vifaa kwa ajili ya zahanati hiyo pamoja na kuleta madaktari na wauguzi ikiwemo kumalizia  ujenzi wa choo cha nje kinachojengwa na wananchi ili waweze kupata huduma hiyo kwa haraka na kuondokana na changamoto zinazowakabili kwa muda mrefu .
Share To:

msumbanews

Post A Comment: