Wednesday, 30 October 2019

PROF. MWAKALILA ASEMA UTUMISHI WA UMMA NI NIDHAMUMkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amewataka watumishi wa Chuo hicho kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa Umma.

Prof. Mwakalila ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Uongozi wa Chuo hicho na wafanyakazi lengo likiwa ni kukumbushana, kuelekezana na kujipanga kwa ajili ya mwaka mpya wa masomo 2019/20.

"Sisi ni watumishi wa umma na Utumishi  wa Umma ni dhamana hivyo tusikubali kuchezea fursa hii tuliyonayo ni vyema tukatimiza Wajibu wetu kwa kufuata kanuni, taratibu na Sheria za Utumishi wa Umma,"anasisitiza Prof. Mwakalila.

Pia Mkuu huyo wa Chuo amewataka wafanyakazi wote kuwa  na uelewa wa dira ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kuwa ni kitovu cha utoaji wa Maarifa bora kuhusu ubunifu, uvumbuzi na kuendeleza Amani na Umoja.

Amesema Chuo hicho pia kina jukumu la kutoa mafunzo ya uongozi na maadili,mafunzo ya Kujiendeleza na Kufanya tafiti zinazotatua changamoto katika jamii.
Akizungumza
Profesa Mwakalila pia ameelezea baadhi ya mafanikio ya Chuo hicho kuwa ni pamoja na kuboresha  mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ambapo tayari  vyumba vyote vya madarasa vimefungwa viti visivyohamishika, Madarasa yamefungwa vifaa vya kisasa vya kufundishia, idadi ya vitabu imeongezwa  kwenye Maktaba kwa kampasi zote mbili, ikiwemo ya Kivukoni na ile ya Karume- Zanzibar.

Mkuu huyo wa Chuo pia amebainisha baadhi ya mikakati ya Chuo hicho kuwa ni  ni pamoja na kuendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ujenzi wa hosteli kwa kampasi ya Karume- Zanzibar na  kuongeza bajeti kwa ajili ya tafiti mbalimbali lengo likiwa ni kutatua changamoto katika jamii.

Prof. Mwakalila amewataka  viongozi wenzake wakiwemo Manibu wa Chuo hicho, Wakuu wa idara na Vitengo katika Chuo hicho kuhakikisha wanatenda haki kwa watumishi walio chini yao ikiwa ni pamoja na kujiepushe na vitendo vyote vya ukabila, dini au Rangi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
30/10/2019

No comments:

Post a comment