Tuesday, 29 October 2019

Benki ya CRDB yakabithi pikipiki tano zenye dhamani ya shs 10 milioni kituo cha polisi Usa River


Happy Lazaro,Arusha.


Benki ya CRDB  imekabithi msaada wa pikipiki  tano zenye thamani ya shs 10 milioni kwa kituo cha polisi USA  river kwa ajili ya kuimarisha doria na usalama wa wananchi na mali zao.

Akizungumza wakati wa kukabithi msaada huo katika kituo cha polisi USA river ,Mkurugenzi wa wateja wadogo na wa Kati katika benki hiyo,Boma Raballa alisema kuwa,benki hiyo inatambua na kuthamini sana umuhimu wa usalama wa raia na Mali zao na hivyo wamekuwa wakishirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Raballa alisema kuwa,utoaji wa msaada huo ni  muendelezo wa utekelezaji wa mpango mkakati wa benki hiyo wa kusaidia huduma za kijamii kupitia sera ya kusaidia jamii ,na kwa kufanya hivyo jeshi hilo litaweza kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi na kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zake kwa kufanya doria katika maeneo mbalimbali.

"benki ya CRDB  kwa kutambua umuhimu wa jeshi hilo ikiwa sehemu ya jamii na mdau mkubwa wa maendeleo imekuwa ikichangia katika kuboresha utendaji wa jeshi la polisi  katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi Marangu Kilimanjaro,pamoja na ununuzi wa gari kwa ajili ya kituo hicho na maeneo mengine  mbalimbali hapa nchini "alisema  Raballa.

Naye Meneja wa kanda ya kaskazini wa benki hiyo,Chiku Issa alisema kuwa,watahakikisha wanafanya  kazi kwa ushirikiano  na jeshi hilo  katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili  ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Chiku alisema kuwa,wamefikia  hatua ya kusaidia usafiri  huo kutokana na changamoto ya usafiri inayowakabili ,jambo ambalo limekuwa likipunguza ufanisi wa utendaji kazi kwa askari  hao na hivyo pikipiki hizo zitasaidia sana kuongeza ufanisi kazi kwa  wakati katika jeshi hilo.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru ,Jerry Muro alishukuru benki hiyo kwa msaada mkubwa wa usafiri huo wa pikipiki kwa askari wake  ambao sasa umewezesha kuzinduliwa rasmi kwa zoezi la kwanza la doria ya pikipiki katika wilaya hiyo.

Muro alisema kuwa, msaada wa pikipiki hizo utasaidia sana kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi katika wilaya hiyo kwa kufanya doria katika vichochoro mbalimbali ambavyo vilikuwa havifikiki kwa haraka , pamoja na kusimamia  usalama barabarani  .

Aidha Muro aliwataka askari  polisi kuzitumia  pikipiki hizo kwa malengo yaliyowekwa badala ya kuzitumia kwa maslahi yao binafsi ,huku wakihakikisha ulinzi unaimarishwa katika maeneo mbalimbali kwa kutumia vitendea kazi hivyo .

Mwisho.

No comments:

Post a comment