Waziri wa Elimu sayansi na Teknolojia Prof,JOYCE NDALICHAKO  ameutaka uongozi wa Benki ya biashara ya Mwalimu MCB BANK kuboresha huduma za kifedha ikiwemo kuweka vivutio na masharti rafiki ambayo yatawawezesha walimu nchini kukopa fedha ili kukuza vipato vyao.

Prof,Ndalichako ametoa wito huo wakati akifunga Kongamano la  walimu
wilayani Kasulu Mkoani Kigoma na kusisitiza kuwa matarajio ya serikali  ni kuona benki ya biashara ya mwalimu inakuwa rafiki kwa walimu nchini kwa  kuondoa adha na vikwazo  ambavyo  kwa muda mrefu walimu wamekuwa wakikabiliana Navyo katika taasisi mbalimbali  za kifedha.

"Benki ya Biashara ya Mwalimu  iwe na ahueni kwa mwalimu anapokuwa ni mteja katika kufanya hivyo walimu wengi watahamasika kujiunga na benki hii, kupitishia mishahara pamoja na hata kuchukua mikopo"

Aidha  ameutaka uongozi  wa Benki hiyo  kusimamia vizuri fedha iliyokwisha wekezwa na walimu ili kuwavutia walimu wengine ambao bado hawajajiunga na kusisitiza kasi ya  uanzishwaji wa ofisi za benki hiyo katika mikoa yote nchini iongezeke ili kuwavutia wateja.

" Nafahamu kwamba tayari  mnatoa huduma kidijitali na mnashirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma katika maeneo ambayo hamna ofisi na lakini ni muhimu mkaharakisha uanzishwaji wa ofisi zenu kila mkoa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma,,

Waziri Ndalichako pia amewaasa walimu nchini kuwa na Utamaduni wa kujiwekea akiba pindi wanapopata mishahara yao ili iwasaidie kuanzisha miradi mingine ya kiuchumi ambayo itakuwa mkombozi wa maisha yao pindi wanapostaafu.

""Walimu tambueni akiba ni kile kitu unachokiweka kwanza kabla ya kuanza matumizi, lakini watu wengi wanadhani akiba ni bakaa baada ya matumizi kwa utaratibu huo kamwe hakutakuwa na kitu kinachobaki,,

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Mwalimu  Richard  Makungwa
amesema benki hiyo ime endelea kujiimarisha katika kusogeza  huduma kwa wateja wake nakwamba  tayari imeanzisha ofisi zake katika baadhi ya mikoa nchini  ikiwemo  MBEYA MOROGORO na MWANZA   huku ishirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma kwa wateja ambao bado mikoa yao haijafikiwa.

Amesema katika benki hiyo mwalimu mmoja mmoja anamiliki hisa takribani asilimia 35.28 huku chama cha walimu na kampuni yao wakimiliki takribani asilimia 16.17.

" ukiangalia utakubaliana nami kuwa chombo hiki ni cha walimu na madhumuni yake ni kuwaletea maendeleo wao wenyewe ndiyo maana tukasema lazima tuwafikia walimu popote walipo ,,alisema Mkurugenzi huyo.

Naye mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange amesema mara nyingi watumishi wanakosa nidhamu ya fedha na kutumia zaidi ya kile anachopata na kusisitiza kuwa ni vizuri walimu wakawa na utaratibu wa kujiwekea akiba ili pindi wanapostaafu waweze kuishi maisha ambayo wanaishi wakiwa kazini.

 Nae mwalimu mstaafu aliyeshiriki kongamano hilo Kalist Tarimo ameishukuru Benki ya Biashara ya Mwalimu kwa kufanya Kongamano hilo ili kutoa elimu kwao lakini pia ameishaiuri benki hiyo kuwana na ofisi katika kila Wilaya ili walimu waweze kutumia huduma za benki hiyo.

Kongamano hilo limeandaliwa na Benki ya Biashara ya Mwalimu na limeshirikisha walimu kutoka Mkoa wa Kigoma.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: