Zao la mkonge miaka miwili iliyopita liliwakusanya wadau wa mkonge duniani kote na kufanya Kongamano hoteli ya Tanga Beach Resort jijini Tanga, Tanzania, huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Kilimo (wakati huo), Dkt. Charles Tizeba. Pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Ltd (kushoto), na mbele yake ni Meneja Mahusiano wa Kampuni ya Katani Ltd Theodora Mtejeta wakiwa na wadau wengine wa mkonge. (Picha na Yusuph Mussa).

Na Yusuph Mussa, Tanga

 Mtendaji wa Kampuni ya Katani Limited Juma Shamte amesema changamoto zinazotokea kwa sasa kwenye Mfumo wa Wakulima Wadogo wa Mkonge kwenye Vyama vya AMCOS katika mashamba ya Mwelya, Magunga, Ngombezi, Magoma na Hale unachangiwa na uchanga wa wataalamu, watendaji na usimamizi katika fani ya Mkonge.


Moja ya changamoto hizo ni zile zilizotolewa na wakulima na wafanyakazi kwenye ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kissa Kasongwa Septemba 2, mwaka huu ikiwemo kudai mkonge wao unavunwa mwingi, lakini kiasi cha fedha wanachopata ni kidogo, lakini wengine wakidai mkonge wao hauvunwi kwa wakati, na hata ukivunwa haupelekwi kiwandani kwa muda muafaka, na wakati mwingine unaachwa shambani na kuharibika.


Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi akiwa ofisini kwake jijini Tanga, na kuongeza kuwa ni muhimu wadau wa mkonge kuweza kusaidia mfumo huo kukaa sawa ili watu wasije wakakata tamaa kwenye zao la mkonge, ama mfumo huo ukashindwa kuwa endelevu.


"Usimamizi wa kazi za mkongeni ni mfumo uliojengwa. Ili kujenga mfumo huo kunahitajika taaluma na uzoefu. Watu muhimu kwenye mfumo huo ni Bwana Shamba, Mhasibu na Bwana Fundi. Wanatakiwa wapate mafunzo yasiyopungua miaka miwili, na baada ya hapo wanakuwa na taaluma na vyeti. Hivyo mpaka anakuwa msimamizi atakuwa na taaluma ya vitendo na darasani, na kumuwezesha kusimamia vizuri.


"Moja ya masharti ya usimamizi, ni kupima matarajio ya mavuno ya shamba la mkulima (field test), ratiba ya kukata mkonge (cutting programme), lakini kujua mkonge utatoa singa (meta kwa tani) kiasi gani. Na jambo hilo linafanyika kabla, na kumshirikisha mkulima ama mwakilishi wa chama (AMCOS). Kwa sasa jambo hilo la usimamizi lipo kwa chama, na kwa sasa suala hilo halipo ama halifanyiki kama taaluma inavyoelekeza" alisema Shamte.


Shamte alisema kwa kutofuata taratibu hizo za usimamizi na kitaaluma, kunatoa mwanya wa kufanya makosa na udanganyifu, na kusababisha kilio kwa wakulima. Na kuongeza hizo ndiyo kazi zilikuwa zinafanywa na Katani Limited kuhakikisha kazi zinafanyika bila malalamiko.


Shamte alisema kilimo cha mkonge ni cha biashara, na mfumo wa ushirika ulivyo sasa, unakinzana na mahitaji ya soko na ushindani wa kwenye soko, hivyo sheria ya ushirika ipitiwe ili iweze kuendana na soko.


Shamte alisema Kampuni ya Katani inaendelea kutoa huduma, lakini ikitaka suala la malipo ya mkonge lisichelewe. Na pia suala la kodi kati ya Katani na AMCOS hasa kwenye suala la VAT liwekwe vizuri, kwani Kampuni inalazimika kulipa kodi ambayo ilipaswa kulipwa na mkulima kupitia AMCOS.


Mwenyekiti wa Ushirika wa Wakulima wa Mkonge Magoma (AMCOS) Abdi Shekighenda alikiri kuwa kama AMCOS zitashindwa kuajiri watendaji wenye taaluma ya usimamizi wa mkonge, wakulima wanaweza kupata hasara kwa kuweza kupoteza mkonge ukiwa shambani ama kupunjwa fedha zao, lakini wao Magoma wanaajiri watu wenye weledi, huku wakivuna mkonge kwa utaratibu unaotakiwa.


"Sisi AMCOS za Mkonge Katiba yetu ni moja, nayo ni kumnufaisha mkulima. Ili kuondoa mkanganyiko ama kufanya kazi chini ya kiwango, tunaajiri wasimamizi wenye diploma ya kilimo na wahasibu wenye diploma. Mpaka sasa tunafuata taratibu za uvunaji vizuri. Mpaka sasa tumewavunia wakulima 143 kati ya 150. Na baada ya kukamilisha hawa saba waliobaki, tutaanza mzunguko wa pili. Hata DC alipokuja kwenye shamba letu, aliona kazi nzuri iliyofanywa na AMCOS" alisema Shekighenda.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela, Agosti 21, mwaka jana, alibadili muundo wa Wakulima wa Mkonge chini ya mfumo wa SISO kwenye mashamba ya Magunga, Magoma, Hale, Ngombezi na Mwelya. Ni baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima wa mkonge, kuwa aliyepewa dhamana ya kuwaongoza Kampuni ya Katani Ltd, anachelewesha malipo ya wakulima na wafanyakazi.


Ndipo Shigela kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali akaamua wakulima watajisimamia wenyewe kupitia AMCOS zao kwenye kukata mkonge hadi kuuza, tena kwa mnada. Na Katani Ltd atabaki kama msindikaji tu wa zao hilo, na yeye akilipwa na AMCOS kwa kazi ya usindikaji.


MWISHO.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: