Wananchi wa Kijiji cha Lorbene, Kata
ya Msitu wa Tembo, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wakiwa kwenye picha ya
pamoja na mfadhili aliyewachimbia kisima kirefu, Said Nassoro maarufu mzee
Mwarabu (mwenye fulana ya mistari miekundu katikati). Ni baada ya wananchi hao
kuandamana hadi Kitongoji cha Nyorinyori wakitokea Kijiji cha Lorbene, kama
ishara ya kutoa shukrani kwa kupata kisima hicho kilichogharimu sh. milioni 30.
(Picha na Yusuph Mussa).
Na Yusuph Mussa, Simanjiro
WANANCHI wa Kijiji cha Lorbene
katika Kata ya Msitu wa Tembo, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamesema sasa
shughuli za maendeleo zitakwenda kwa kasi baada ya wananchi hao kupatiwa maji
ya kisima kirefu kilichogharimu sh. milioni 30.
Katika kuonesha furaha yao ya kupata
maji, viongozi wa jamii ya kimasai maarufu kama Laigwanani wa kijiji hicho,
wamefunga safari kwenda kumpa shukrani mwekezeji Said Nassoro anaechimba madini
Kitongoji cha Nyorinyori katika Kijiji cha Lorbene, kwa msaada wa kuwachimbia
kisima cha maji wananchi wa eneo hilo.
Viongozi hao wa jamii ya kimasai
wametoa shukrani hizo hivi karibuni kwa mwekezaji huyo baada ya
kutatua changamoto ya maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo yao
ambapo kabla ya msaada huo, wananchi hao walikuwa wakipata maji kwa kusafiri
zaidi ya kilomita 20, kwenda kwenye vyanzo vilivyopo milimani, jambo ambalo
iliwabidi akinamama kuamka saa 10 usiku na kusafiri kwa usafiri wa punda na
kurudi nyumbani usiku wa manane kesho yake.
"Tunashukuru kwa msaada huu wa
kuchimbiwa kisima cha maji, kwani tulikuwa tunasafiri umbali mrefu zaidi ya
kilomita 20 kutafuta maji. Wake zetu walikuwa wanasafiri na punda kwenda
milimani, wanaondoka usiku wanarudi kesho usiku, hivyo tunamshukuru mzee
Mwarabu kwa kisima hiki" alisema Kipara Simangu, Laigwanani wa Lorbene
Simangu, mbali na kutoa shukrani
hizo, viongozi hao wa kimasai wametoa wito kwa wawekezaji wengine kuiga moyo
huo wa upendo aliouonesha Nassoro kwa kusaidia jamii kwa hiari yake
mwenyewe.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha
Lorbene, Elisha Njaram alisema changamoto ya maji kwenye kijiji hicho ilikuwa
kubwa, lakini sasa wananchi wataachana na kutafuta maji mbali, na kujikita
kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
Mwekezaji Nassoro maarufu kama mzee
Mwarabu, alisema ataendelea kutoa misaada ya kuchimba visima vya maji kwa jamii
zinazozunguka eneo hilo linalokaliwa na jamii za wafugaji wa kimasai kadri
atakavyoweza kwa kuangalia mahitaji muhimu ya binadamu hasa kwa jamii zilizo
mbali na miundombinu ya maji.
Aidha, Nassoro ambae ni mkazi wa
Arusha, pia ameweza kuchimba visima viwili vyenye urefu wa zaidi ya mita 180
vilivyogharimu sh. milioni 60 kwenye Kijiji cha Kitwai wilayani Simanjiro kwa
ajili ya wananchi na kuvikabidhi kwa Serikali ya kijiji.
Wilaya ya Simanjiro ambayo ni
miongoni mwa wilaya zenye maeneo makubwa zaidi kijiografia nchini, imekuwa
ikikabiliwa na uhaba wa maji hasa katika maeneo mengi ambayo hukaliwa na jamii
za wafugaji pamoja na wanyama pori.
MWISHO.
Post A Comment: