Waganga wakuu wa Mikoa Tanzania Bara wamepewa mwezi mmoja kuhakikisha kuwa wanazifanyia tathmini ya kina Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya zao kuona kama zinaendana na kasi ya mabadiliko yanayokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Agizo hilo limetolewa jana mjini Songea na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji Huduma za Afya ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na Wajumbe wa Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya kutoka Halmashauri ya Namtumbo, Halmashauri ya Wilaya ya Songea pamoja na Manispaa ya Songea.

Amesema anawapa siku 30 Waganga Wakuu wa Mikoa yote kuhakikisha kuwa wanafanya tathmini ya Wajumbe waliopo katika ofisi zao kama wanatosha kuendelea na nyadhifa zao za kusimamia jukumu la uendeshaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri zao.

Dkt Gwajima ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa baadhi ya Wajumbe wa Kamati hizo hawana sifa zinazowafanya kushindwa kutekeleza majukumu yao ya usimamizi na uendeshaji huduma za afya katika maeneo yao, Waganga Wakuu wa Mikoa watalazimika kuwaweka pembeni Wajumbe hao na kuunda upya Kamati ambazo zitaweza kuiendeleza agenda ya mabadiliko katika sekta ya afya.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: