“KAMA kuna pesa imetumwa kimakosa kwenye simu yako, hata kama mwenye simu aliyekutumia kimakosa atakuomba na kukubembeleza, usimrudishie yeye, bali ziache na uijulishe kampuni ya simu inayohusika wao ndio wamrudishie.”

Tahadhari hiyo ilitolewa na Mtakwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Batholomew Marcel aliwatahadharisha Watanzania kuwa makini kwani hali hiyo inaweza kuwasababishia hasara na pengine kuwaingiza katika mikono ya sheria za nchi kama tuhuma za uhalifu mwingine wowote, licha ya nia nzuri inayoweza kuwapo kwa mrudisha pesa.

Alisema inayepokea pesa iliyotumwa kwake kimakosa anapaswa kuijulisha kampuni husika ya simu vinginevyo anaweza kujikuta anafanya malipo na kutuma pesa kwa wahalifu huku mifumo ikionesha pesa ilikwenda kwake.

Alisema kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), watu wengi wanatumia simu kutunza, kupokea na kutuma pesa zao hivyo, mikakati bora zaidi haina budi kuwapo ili kuepusha uhalifu wa kimtandao hususani kuhusu pesa mtandao.

“Hapa lazima kuwa makini kwani teknolojia hii ya pesa mtandao pia ina changamoto nyingi na hatari. Kazi ya kurudisha pesa kwa aliyetuma kimakosa, iache ifanywe na kampuni husika ya simu yaani mtoa huduma sio wewe,” alisema.

Changamoto nyingine Marcel alisema ni pamoja na kuibuka wimbi la matapeli wanaojifanya kumfahamu mtu huku wenyewe wakijifanya ni wanasiasa, viongozi wa kikazi, kiserikali, kidini au wanafamilia wanaotoa maelekezo ya kumtaka mtu afanye malipo, kutuma pesa au kuhitaji msaada kwa ulaghai.

Aliwataka watumiaji wa huduma hizo kuwa makini kwani makosa ya kimtandao ni makosa kama yalivyo mengine na yana sheria zake ikiwamo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Akasema, “Epuka kutunza pesa nyingi katika chombo kimoja kama simu, ukipoteza simu toa kwanza taarifa kwa kampuni husika ya simu ili waifunge kisha sasa, toa taarifa polisi na pia, badili password (namba ya siri) mara kwa mara walau kila baada ya siku 90.”

Akaongeza, “Wengine wanaokumbwa au kulizwa na changamoto za pesa mtandao, ni wale wanaokubali kuaminishwa kuhusu kuwapo biashara inayozaa faida kubwa kwa muda mfupi, kushinda bahati nasibu hata ambazo hawakushiriki na kupata mikopo kirahisi, lakini wakatakiwa kutanguliza malipo,” alisema.

Akasisitiza, “Kuwa makini kwa kuepuka mikopo au dili zinazokutaka kutanguliza fedha…” Kwa upande mwingine, alisema zipo fursa nyingi za mitandao ikiwamo kufanya malipo mbalimbalimbali yakiwamo ya huduma za kijamii kama maji, umeme na ankara nyingine; pamoja na biashara huku wengine wakijiajiri au kuajiriwa katika sekta hiyo ya pesa mtandao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: