NAIBU Waziri wa Kilimo Omar Mgumba

Na Yusuph Mussa, Kilindi

 NAIBU Waziri wa Kilimo Omar Mgumba amesema pamoja na jitihada za wananchi kulima mazao ya kila aina, lakini bila mazao hayo kufikishwa sokoni kwa urahisi ni kazi bure. Hivyo amelichukua tatizo la barabara ya kutoka Handeni hadi Kilindi kama jambo linalotakiwa kufanyiwa kazi haraka.


 Amesema kutokana na kujengwa Bomba la Mafuta kati ya Hoima, nchini Uganda hadi Chongoleani, mkoani Tanga, ni vizuri kukawa na barabara ya lami ili iende sambamba na bombo hilo kutoka Handeni- Kiteto mkoani Manyara- Kondoa mkoani Dodoma hadi Singida yenye urefu wa kilomita zaidi ya 450, huku upembuzi yakinifu ukiwa umekamilika, na barabara hiyo ipo kwenye Ilani ya CCM kwa takribani miaka 10 sasa.


 Aliyasema hayo Mei 25, 2019 kwenye uzinduzi wa zao la muhogo kitaifa lililofanyika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, huku akiweka msisitizo kwa wadau wa muhogo waweze kuwasaidia wakulima kwa kujenga viwanda vya kuchakata zao la muhogo kabla ya kusafirishwa sokoni ndani na nje ya nchi.


    "Suala la barabara kati ya Handeni hadi Songe (kilomita 120) yalipo Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi ni changamoto ya kweli. Ili mazao ya wakulima wetu yaweze kufika sokoni kwa urahisi ni lazima tuboreshe barabara zetu. Hivyo nalibeba hili ili kwenda kufanyiwa kazi. Najua kuna Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga. Na bomba hili litapita maeneo haya. Na kwa vile tayari kuna mpango wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Handeni hadi Singida, kutaongeza tija kwa wakulima wetu.


    "Na niseme hapa, soko la muhogo halina shida, lipo ndani na nje ya nchi, lakini kinachohitajika ni viwanda vingi vya kuchakata muhogo huo ili uende sokoni ukiwa umekaushwa kabisa. Kilo moja ya muhogo mbichi ni sh. 100, lakini kilo moja ya muhogo uliokaushwa ni sh. 300, yaani kilo tatu za muhogo mbichi ni sawa na kilo moja ya muhogo uliokaushwa. Hivyo kukiwa na viwanda vingi hapa Kilindi maana yake wakulima wetu watapata faida" alisema Mgumba.


 Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini (CCM) Daniel Nswanzugwanko ambaye aliongozana na Mgumba kama mdau wa muhogo, alisema barabara ya kutoka Handeni hadi Songe inaweza kuwa kikwazo kwa wakulima wa wilaya ya Kilindi, kwani hata walime kiasi kikubwa, lakini kama barabara mbovu hawawezi kuuza mazao yao kwa tija, na wafanyabiashara watanunua kwa bei ya chini kwa kisingizio cha barabara.


    "Kasulu tunashida ya barabara lakini kwa hii ya kutoka Handeni kuja Kilindi ni mbaya zaidi. Msitarajie wakulima kupata tija kwa barabara hii. Hata walime kwa kiwango gani, hawawezi kufanikiwa. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, nakwenda kulisemea hili kwa kwa nguvu na uzito wa kipekee, kwani kwa hali niliyoiona leo, wenye magari hawawezi kuleta magari, na nimeona baadhi ya magari yameanguka njiani na mengine kukwama" alisema Nswanzugwako, huku wananchi wakilipuka kwa shangwe ndani ya Ukumbi wa Halmashauri ya Kilindi.

 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu na Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM) Mahamoud Mgimwa, aliwataka wananchi wasimuhukumu Mbunge wa Jimbo la Kilindi Omar Kigua kwa ubovu wa barabara, kwani tatizo hilo lipo nchi nzima hasa wakati huu wa mvua za masika, na yeye atakwenda kulisemea bungeni ili kuweka msisitizo wa kujengwa kwa barabara ya lami kati ya Handeni hadi Songe kilomita 120, ambayo imeshafanyiwa upembuzi yakinifu zaidi ya miaka mitano iliyopita.


  Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Gratian Makota alimueleza Mgumba kuwa halmashauri hiyo imewahamasisha vya kutosha wakulima katika kuachana na jembe la mkono, kwani katika matrekta 15 aina ya Ursu yaliyoletwa mkoa wa Tanga na Shirika la Maendeleo (NDC), matrekta 13 yamekopwa na wakulima wa Kilindi, na kwa sasa shirika hilo pamoja na mkopaji ndiyo wanajadiliana namna ya kurejesha mkopo.

Nao wakulima walimuomba Naibu Waziri kwenda kuwaombea kwa Shirika la NDC warejeshe mkopo baada ya miaka mitatu badala ya miaka miwili, kwani walichukua matrekta hayo wakiwa wamepitwa na msimu mmoja wa kilimo, na hiyo ni kutokana na kukosekana kwa mvua kwa wakati.


    MWISHO
Share To:

Post A Comment: