Sunday, 26 May 2019

HALMASHAURI YA MJI WA MAFINGA YAPATA HATI SAFI KUTOKA KWA CAG

Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Zakaria Vang’ota akiwa sambamba na kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Mafinga Francis Maghembe waalisema kuwa kupatikana  kwa hati safi katika Halmashauri hiyo kutachochea zaidi kasi ya utendaji kazi ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa
 
 Baadhi ya madiwani na watendaji wa halmasahuri ya Mji wa Mafinga wakifuatilia kwa umakini ripoti ya CAG wakati wa baraza maalum la halmashauri hiyo

 NA FREDY MGUNDA,MAFINGA.
 
HALMASHAURI ya mji wa Mafinga imefanikiwa kupata hati safi kutokana na utendaji bora,usimamizi wa miradi ukusanyaji mapato  kwenye vyanzo vyake vya ndani  katika kipindi cha mwaka 2018-2019.

Akizungumza kwenye kikao maalumu cha  baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kwa lengo la kusoma rasmi taarifa  ya CAG kwa niaba ya mkuu wa mkoa, Kaimu Katibu tawala wa mkoa wa Iringa, Lucas Kambelenje alisema Halmashauri hiyo imeweza kupata hati safi katika kipindi cha mwaka 2018 -2019 kutokana na watendaji wake wakiwemo madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano katika suala zima la kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na kipindi cha nyuma.
‘’Nawapongeza watendaji wa Halmashauri na madiwani kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kufanikiwa kupata hati safi, hivyo nawapongeza muongeze kasi zaidi kiutendaji na kamwe msibweteke,’’alisema

Aidha aliwataka kufuata misingi imara itayowawezesha kudhibiti mapato na matumizi ya halmashauri kwa kuondoa mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi cha nyuma kama kuchelewa kuwasilisha mahesabu kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG) ,kuchelewa kuwasilisha taarifa za matumizi  bila ya kuwa na viambatanishi vya malipo .


‘’Pia epukeni kulipa madeni hewa kwa watumishi ama  waliokufa,kuacha kazi ama watumishi watoro sehemu za kazi, kwani kufanya hivyo kutapelekea halmashauri kupata hati chafu.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Zakaria Vang’ota alisema kuwa kupatikana  kwa hati safi katika Halmashauri hiyo kutachochea zaidi kasi ya utendaji kazi ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

‘’Ni dhahiri kila diwani atatekeleza majukumu yake ili kuweza kudhibiti mapato na matumizi ya halmashuari ma kuweza kufanya vizuri zaidi,‘’alisema Vang’ota.


Hata hivyo Vang’ota aliwahimiza madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na kuwataka kuwatendea haki wananchi ambao wamewachagua kwa kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa kuwatataulia kero zinazowakabilia.

Akizungumzia hoja hizo kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Mafinga Francis Maghembe alisema kuwa watahakikisha hoja zote zinafanyiwa kazi ili kusijitokeze hoja nyingine au kuongezeka kwa madeni ambayo halmashauri inadaiwa.

No comments:

Post a comment