Saturday, 6 April 2019

ZAIDI YA WAUMI 2000 WA KANISA JESUS SALVATION WAKOSA ENEO LA KUABUDIA

Askofu wa Kanisa hilo Rejina Akaro akionyesha vielelezo vya eneo lake

ZAIDI ya waumini 2000 wa Kanisa la Jesus Salvation la Jijini Tanga hawana mahala pa kufanyia ibada kutokana katazo lililowekwa na Serikali la kuzuia ujenzi wa kanisa hilo na kuharibu miundombinu ya ujenzi wa awali.

Kufutia hatua hiyo amemuomba Rais Dkt John Magufuli kuingilia kati suala hilo kumsaidia ili aweze kupata haki yake ya kutumia eneo hilo ambalo ni mali yake kwa ajili ya kufanyia ibada.

Hayo yalisemwa na Askofu wa Kanisa hilo Rejina Akaro wakati akizungumza na mtandao huu mara na kueleza kilio hicho na kubainisha adha wanayoipata waumini wake na kufikia hatua ya
kufanyia ibada nyumbani kwake eneo la uwani kutokana na mgogoro uliopo
katika eneo la ujenzi wa kanisa hilo.

Kwa mujibu wa Askofu huyo alisema mgogoro wa Kanisa hilo lililopo eneo la Sahare kata ya Mzingani Jijini hapa ambalo anadai alilinunua miaka 25 iliyopita na kuamua kulitoa kwa ajili ya kanisa jambo ambalo limemuingiza katika mgogoro na mamlaka za Jiji.

Alisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu huku hakuna hatua zozote zinazochukuliwa ili kuweza kuwanusuru waumini hao ambao wanahangaika kwa ajili ya kupata eneo la kufanyia ibada kama ilivyo kwa dini ama madhehebu mengine.

“Nasikitika sana waumini wangu walikuwa zaidi 2000 lakini sasa nimebakia na waumini 20 tu ndio wanofika nyumbani kwangu huku tukifanya ibada uwani kwangu na kufanya hivi ni kutunyima uhuru wa kuabudu ikiwa tunawekewa kizuizi katika eneo letu ninamuomba Rais Magufuli aingilie kati jambo hilo”Alisema Askofu Akaro.

Alisema mgogoro katika eneo hilo umeanza baada ya kubadilisha matumizi ya kawaida kwenda katika matumizi ya kanisa jambo ambalo limeonekana kutengenezwa na baadhi ya majirani zake ambao anadai wamekuwa na uwezo kifedha katika eneo hilo ambao wanaonekana kutokupendezwa na uwepo wa kanisa hilo.

Askofu Akaro alisema hivi karibuni Waziri wa Ardhi alifanya ziara Jijini hapa na kuzungumza na wananchi juu ya kero zao zinazohusu ardhi lakini cha ajabu alijibiwa kuwa matatizo yake yapo kwa Mkuu wa Mkoa Tanga ambae anaweza kuyashughulikia .

Alisema awali mamlaka za Jiji zilionyesha kuwa eneo hilo ni la wazi lakini kwa mujibu wa Waziri mwenye dhamana eneo hilo ni la makazi hivyo mmiliki anatakiwa kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa ambae swala hilo lipo mezani kwake.

“Ninamashaka sana juu ya majibu ninayopata kuhusiana na mgogoro huu kutokana na kila kiongozi ninaekutana nae anamtupia mpira mwenzake hii pekee inanipa sura mpya kuwa kuna kitu kinaendelea bila ya mimi kutambua na naiomba Serikali iangalie kilio cha waumini wangu”Alisema.

Hata hivyo alimemuomba Rais kuangalia kwa makini juu ya wateule wake kutokana na maamuzi wanayoyachukua dhidi ya migogoro mbalimbali ambapo inaonekana inakwenda kinyume chake na hivyo kuwafanya wananchi kuichukia serikali .

Mwisho.

No comments:

Post a comment