Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Bibi Jenista Mhagama kukutana na mawaziri wa sekta nyingine ili kutafuta namna ya kuondoa mkanganyiko uliopo kwenye vyombo vya udhibiti hapa nchini.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Alikuwa akitoa ufafanuzi juu ya masuala yaliyogusa vyombo vya udhibiti kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka nyingine za udhibiti pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), OSHA, BRELLA na Taasisi ya Mionzi ambayo yaligusiwa na Waheshimiwa Wabunge.

Alisema licha ya Serikali kujenga mazingira wezeshi na rahisi ya kufanya biashara na uwekezaji, bado kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji kama walivyoeleza Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuchangia hoja hiyo.

“Changamoto nyingine ambayo imeonekana kuwa kikwazo cha biashara na uwekezaji ni muingiliano wa majukumu ya taasisi hizo. Kwa mfano, uwepo wa majukumu yenye kufanana kwa TFDA, TBS, Mkemia Mkuu wa Serikali, Bodi ya Maziwa, Bodi ya Nyama, Baraza la Mifugo, EWURA, SUMATRA na TANROADS ni kikwazo kikubwa katika kurahisisha mazingira ya kufanya biashara,” alisema.

Alisema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu mamlaka hizi na namna ya utendaji kazi wake. Miongoni mwa kero hizo ni mchakato wa muda mrefu wa kupata leseni za biashara; gharama za usajili wa bidhaa zinazotozwa na TFDA; suala la viwango vya TBS; madai ya kuwepo kwa unyanyasaji unaofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kushirikiana na polisi dhidi ya wafanyabiashara.

Pia walibainisha changamoto nyingine kuwa ni umbali wa kutoka makao makuu na maabara za taasisi ya mionzi hadi eneo wanalofanyia kazi kama vile bandari na viwanja vya ndege.

“Tayari nimeshatoa maelekezo na yameanza kufanyiwa kazi na Waheshimiwa Mawaziri wa sekta husika chini ya uratibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) kwamba wakae pamoja kupitia sheria na mgawanyo wa majukumu wa taasisi za udhibiti ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa” alisema.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza mawaziri husika wahakikishe kuwa wakuu wa Mamlaka ya Mapato na taasisi zake, wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia sheria bila kuwabughudhi wafanyabiashara na wawekezaji.

Wakati wa mjadala huu, wabunge 142 walichangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kati ya hao, wabunge 98 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja bungeni na wabunge 44 walichangia kwa njia ya maandishi.

Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/- kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo sh. 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo
Share To:

msumbanews

Post A Comment: