Na EZEKIEL NASHON, KONGWA.

KUELEKEA uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, Vijana wametakiwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali  mbali katika uchaguzi huo ili waweze kushika nyadhifa mbali mbali.

Wito huo umetolewa Wilayani Kongwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM, Mkoa wa Dodoma, Billy Chidabwa, wakati wa ziara ya kamati ya utekelezaji ya UVCCM walipotembelea Wilaya hiyo.

Amesema vijana wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi ili kushika nyadhifa mbalimbali ili wawe na maamuzi katika  ngazi za juu wasibaki kulalamika kwani wao ndio tegemeo la Taifa.

“Vijana wenzangu mwaka huu tunaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani niwaombe mjitokeze kwa wingi kwani nyie ndio nguzo na ndio taifa la leo, hivyo jitokezeni kwa wingi  kugombea nafasi mbalimbali na  msibaki kulalamika kutokushirikishwa katika maamuzi hivyo jitokezeni” amesema Chidabwa.

Aidha  amesema wao kama jumuiya ya vijana wataendelea kuwa mawakili wazuri katika kutatua kero mbalimbali kwa wananchi, na kuwa chombo cha kuwasemea katika ngazi mbalimbali serikalini.

Pia amewataka vijana kujenga utalatibu wa kuhoji utekelezaji wa ilani pale  wanapoona hawajaridhishwa na baadhi ya vitu.

“Ndugu zangu serikali  ya sasa ni ya uwazi na ukweli hivyo vijana jitokezeni kuhoji  utekelezaji wa  ilani, pale mnapoona hamjaridhishwa katika sehemu flani msinyamaze jitokezeni mhoji juu ya jambo  hilo serikari ya sasa ni  uwazi na ukweli” amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu anaewakilisha kundi la vijana Mariam Ditopile  amebainisha kuwa lengo la ziara  hiyo ni kuangalia utekelezaji wa ilani ya chama, kama yale wanayoyapanga katika ngazi mbalimbali yanatekelezwa katika ngazi za chini, na kuangalia asilimia ya halmashauri kwa vijana kama inawafikia.

“Ziara hii tunazunguka tarafa zote  za mkoa wa Dodoma lengo tunataka  tuangalie utekelezaji wa ilani, kwa sababu kule bungeni tunapanga mikakati mingi sasa kama vijana tumekuja kuangalia je yanawafikia wananchi na kunufaika” amesema Mariam.

Pia tunatenga asilimia kwa vijana kwa kila halmashauri tumekuja kuangalia je halmashauri zinatenga na vijana wananufaika,lengo ni kuwa kwamua vijana kiuchumi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: