Rais Dkt. John Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mbeya kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inatekeleza ahadi zote zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ili kujenga Tanzania bora zaidi.

Magufuli amesema hayo leo tarehe 25 Aprili, 2019 muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe Mkoani Mbeya akitokea nchini Malawi alikokuwa katika Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais wa Malawi Prof. Arthur Mutharika.

Akiwasalimu maelfu ya wananchi wa Jiji la Mbeya waliojitokeza kumpokea kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Mbalizi, Iyunga, Nzovwe, Mafiati na Uzunguni, Magufuli amesema utekelezaji wa ahadi hizo unakwenda vizuri na ametaja baadhi ya maeneo yenye mafanikio makubwa kuwa ni kuimarishwa kwa huduma za afya ambapo hospitali 67 na vituo 352 vinajengwa nchini kote, kuimarishwa kwa elimu ambapo kila mwezi Serikali inatoa shilingi Bilioni 23.8 kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, kuimarisha barabara zikiwemo barabara za Mkoa wa Mbeya, kuimarisha upatikanaji wa maji na maeneo mengine.

Akiwa Mbalizi wananchi wamemuomba awasaidie kutatua tatizo la maji ambapo baada ya maelezo ya Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa aliyeahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kupeleka maji katika eneo hilo, Rais Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa Wizara ya Maji kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unaanza na wananchi wanaondokana na tatizo la maji linalowakabili.

Aidha, Magufuli amesema Serikali inaendelea kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo havijapata huduma hiyo.

“Nataka niwahakikishie ndugu zangu wa Mbeya, tumejipanga kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na tumedhamiria kuboresha maisha ya wananchi, naomba tuendelee kushikamana kusukuma mbele maendeleo, na maendeleo hayana chama” amesisitiza. Magufuli.

Rais Magufuli kesho ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Luanda Nzovwe Jijini Mbeya.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: