Sunday, 28 April 2019

Ofisa ugavi mbaroni tuhuma wizi wa sarujiOfisa Ugavi Msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Benjamin Mugeta anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za wizi wa saruji.

Takriban mifuko ya saruji 134 kati ya 600 iliyonunuliwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari Bwina inadaiwa kuibwa kabla ya kukabidhiwa kwa shule hiyo.

Inadaiwa ofisa ugavi huyo ndiye aliyesindikiza gari lililobeba saruji hiyo kabla ya kukabidhiwa kwa shule hiyo, lakini kamati ya ujenzi ikagoma kupokea mzigo huo kutokana na kuwa pungufu ya idadi ya mifuko iliyopaswa kupokewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alidai kutokuwa na taarifa za tukio hilo licha ya kuahidi kufuatilia kwa wasaidizi wake.

"Sijapata taarifa za tukio hilo naomba nilifuatilie kujua ukweli wake tafadhali," alisema.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mtemi Msafiri, alisema ana taarifa za kuwapo kwa tuhuma hizo na kueleza kuwa wamezikabidhi kwa vyombo vya dola ili zifanye kazi.

"Ndiyo, taarifa tunazo, sisi ndiyo tulioagiza polisi wamkamate kwa mahojiano na hatua zingine za kisheria zichukuliwe kadri watakavyoona inafaa," alidai.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwina, Charles Abel, alidai kamati ya ujenzi haikupokea mzigo huo kutokana na upungufu uliojitokeza.

Alidai mifuko 600 ilipaswa kufika shuleni, lakini ilipelekwa 466, jambo ambalo waliona waliripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.

No comments:

Post a comment