Mratibu wa afya ya mama na mtoto mkoa wa Morogoro Santiel Kinyongoakizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama mkoani Morogoro

Na. Vero Ignatus.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, daktari Kebwe Steven Kebwe amewataka akina mama wajawazito mkoani humo kuzingatia chanjo zote muhimu wakati wa ujauzito ili wajifungue salama.

Daktari Kebwe pia amewataka akina mama hao kuhakikisha watoto wanaowazaa wanapata chanjo zote muhimu katika vituo vya Afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya " Jiongeze Tuwavushe Salama " ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo ya kitaifa Kwa ngazi ya mkoa, Daktari Kebwe amesema  chanjo zinawalinda mama na mtoto atakayemzaa na maradhi mbalimbali yakiwemo pepopunda.

Kuzinduliwa kwa kampeni hiyo katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara ukiwemo wa Morogoro ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali kuu  kwa wakuu wote wa mikoa nchini kuzindua na kutekeleza ajenda ya  kuhakikisha vifo vya wajawazito na watoto wachanga vinapungua.

Daktari Kebwe amesema serikali imewekeza vya kutosha katika sekta ya afya kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana.

Amewataka wanawake wajawazito  wa mkoa wake kuhudhuria kliniki wakiwa na wenza wao na kuhakikisha chanjo wanazipata Kwa sababu zinatolewa bure.

Amesema mama mjamzito anayehudhuria kliniki atajua mapema changamoto za uzazi atakazopitia ili kuepuka uzazi pingamizi, ambao ni moja ya vyanzo vya kifo kwa akina mama, ikiwemo kutokwa damu nyingi wakati na baada ya kujifungua.

Amewataka watendaji wa mkoa, wakiwemo wakuu wa wilaya wote, wakurugenzi, waganga wakuu, wananchi na wanaohusika katika kutoa huduma kuhakikisha vifo vinapungua.

Pia ametia sahihi ya makubaliano ya uwajibikaji wa "kasi" Kwa wakuu wa wilaya zote kuhakikisha maazimio ya kimkoa ya kupunguza vifo yanafikiwa.

" Tunatengeneza utaratibu wa kuwapima ( score card) kuona nani ametimiza wajibu wake ambao kila baada ya miezi 6 utafanyika ," amesema daktari Kebwe.

Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ilizinduliwa na makamu wa Rais, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mwezi November mwaka juzi mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wakuu wote wa mikoa, utekelezaji wake ukiwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto wa mkoa wa Morogoro , Santiel Kinyongo amesema mkoa unafanya jitihada kupunguza vifo vya mama na mtoto, ingawa bado kuna changamoto ndogo ndogo.

Amesema kwa mfano kuna upungufu Wa wakunga katika vituo vya vingi vya mkoa wa Morogoro, isipokuwa Wilaya ya Ifakara na Manispaa ya Morogoro hali inaridhisha.

Pia ameongelea umuhimu wa mama mjamzito kuhakikisha anahudhuria kliniki si chini ya mara 4 wakati wa ujauzito wake ili apate chanjo za kumlinda yeye.

Ameshauri pia mama mjamzito kumpeleka Mtoto atakayemzaa kliniki ili aweze kupewa chanjo zote muhimu.

Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama  inatekelezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo UNICEF

Picha mbalimbali za matukio ya uzinduzi wa kampeni ya Jiongeze tuwavushe salama iliyofanyika mkoani Morogoro
Share To:

Vukatz Blog

Post A Comment: