Serikali imeahidi Kutoa kiasi Cha Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya kujenga na kukarabati Miundombinu mbalimbali katika shule ya msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K Nyerere iliyopo manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako mara baada ya kutii maelekezo yaliyotolewa na Rais John Magufuli ya kuitembelea shule hiyo na kufanya tathmini  kwa lengo la kuikarabati ili  iendane na hadhi ya  Baba wa Taifa.

Waziri Ndalichako amesema, kipaumbele Cha Serikali ya awamu ya Tano ni Elimu, hivyo amemwelekeza Mkuu wa mkoa huo  Adam Malima kuhakikisha kuwa Fedha ambazo zitaelekezwa katika shule hiyo basi zisimamiwe ili zifanye kazi iliyokusiduwa na si kutumika vinginevyo.

“ Rais John Magufuli akiwa katika ziara zake alifika na kuona kuwa shule hii inahitaji kuboreshwa hivyo alinielekeza nifike na kufanya tathmini kwa lengo la kuboresha Miundombinu ya Shule hii, sasa Mkuu wa mkoa mimi na wewe tuhakikishe uboreshaji unafanyika tena kwa kiwango kitakachoendana na hadhi ya Baba wa Taifa letu,” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema fedha hizo zitatumika kujenga mabweni mawili mapya, vyumba vitano vya madarasa, kukarabati Nyumba  za walimu na  kuboresha Miundombinu ya maji.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huo Adam Malima ameahidi kusimamia fedha zitakazotolewa kwa ajili ya kuboresha Miundombinu katika shule
Hiyo na kuwa shule hiyo itakuwa ya mfano na pia ni kumbukumbu nzuri kwa Taifa.

Waziri Ndalichako pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoa huo pia wametembelea Shule ya sekondari ya Ufundi Musoma, Shule ya sekondari Mara na Chuo Kikuu Cha kilimo na Teknolojia Cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani Butiama kwa lengo la kukagua hali ya Miundombinu katika Taasisi hizo.

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
26/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: