Wednesday, 22 August 2018

Watatu Mbaroni Kwa Tuhuma za Mauaji ya Wanawake 9 Jijini Arusha

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limewatia mbaroni watu watatu wanaotuhumiwa kuendesha mauaji tisa ya wanawake katika Mji wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha.

Waliokamatwa ni Richard Msuya(22), Babuu Williamu(24) na Francis Charles(21), wote wakazi wa Kigongoni katika mji wa Mto wa Mbu. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Ramadhani Ng’azi alisema watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani jana kujibu mashitaka ya mauaji.

Kamanda Ng’azi alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kunatokana na jeshi hilo kuendesha msako mkali katika wilaya hiyo na mji huo kwa kushirikisha raia wema. 

Alisema wanawake tisa waliripotiwa kufa katika matukio tofauti katika eneo la Kigongoni Kata ya Mto wa Mbu katika vifo vya utata. 

Miili yao ilikutwa imetelekezwa. Mauaji hayo yalihushisha na vitendo vya ubakaji, ushirikina na uhalifu usio wa kawaida.

Kamanda Ng’azi alisema moja ya matukio ambayo jeshi hilo liliona kama ni ya kulipiza kisasi ni la Julai 10 mwaka huu, ambapo mwili wa mwanamke mmoja wa watoto wawili, Ruth Meena(49) mkazi wa Kigongoni ulikutwa katika mtaro akiwa mtupu akiwa na jeraha kisogoni akiwa ametelekezwa. 

Kamanda Ng’azi alisema kutokea kwa matukio tisa ya mauaji ya wanawake katika mji huo ni jambo la kutisha, hivyo polisi imefanya kazi ya ziada kukabiliana na wahalifu hao.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo na matukio mengine ya kihalifu Polisi mkoani Arusha imeamua kujenga kituo kikubwa cha polisi katika mji wa Mto wa Mbu kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo. 


‘’Tumejipanga kukabiliana na hali hiyo na tunataka kukomesha uhalifu huo wa kuua wanawake katika Mji wa Mto wa Mbu,’’ alisema Ng’azi.

No comments:

Post a comment