Saturday, 14 July 2018

Waziri Mkuu Atembelea Kiwanda Cha Kuchambua Pamba Cha Gaki

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha GAKI na kusema amevutiwa na uwekezaji uliofanywa na wamiliki wa kiwanda hicho ambao ni Watanzania.

“Ninawapongeza wazawa walioamua kujenga kiwanda hiki kwa sababu viwanda kama hivi vinasaidia kukuza kilimo hapa nchini, kiwanda hiki kinachambua pamba na kusindika mafuta,” alisema.

Ametoa pongezi hizo jana jioni (Ijumaa, Julai 13, 2018) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya GAKI Investment pamoja na wananchi waliofika kumsikiliza mara baada ya kukagua utendaji kazi wa kiwanda hicho kilichopo Manispaa ya Shinyanga.

Waziri Mkuu alisema amevutiwa na ujenzi wa kiwanda hicho kwa sababu kinatoa uhakika wa soko la pamba ikizingatiwa kwamba mikoa yote inayolima zao hilo, mwaka huu imezalisha pamba kwa wingi kuliko kawaida.

“Mwitikio wa wakulima wa zao la pamba unaonyesha kwamba bado wana imani na Serikali yao na ndiyo maana nimewaonya wajumbe wa bodi ya SHIRECU kuwa wajihoji kama kweli wameomba nafasi hizo ili kuwatumikia wananchi,” alisema.

“Msije mkadhani kuwa SHIRECU ni mahali pa kuganga njaa. La hasha! Ni mahali pa kukuza soko la pamba. Tunataka viongozi wa sasa watambue kuwa hawajaenda SHIRECU ili kushiba, lazima walete mabadiliko kwenye ushirika na kama hawawezi waachie ngazi,” alisisitiza.

Aliwataka watumishi wa kiwanda hicho wafanye kazi kwa uaminifu na watunze mashine za kiwanda hicho ili kiweze kufanya kazi kwa muda mrefu.

Mapema, akitoa maelezo ya uzalishaji wa kiwanda hicho kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa GAKI Investment, Bw. Gaspar Kileo  alisema kampuni hiyo inajishughulisha na ununuzi wa pamba kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Tabora.

Alisema uchambuzi wa pamba kwenye kiwanda hicho unatumia mashine zenye uwezo wa kuzalisha marobota 400 kwa siku. “Hapa kiwandani pia tunakamua mafuta yatokanayo na mbegu za pamba na tuna uwezo wa kuzalisha lita 10,000 kwa siku,” alisema.

Alisema ili kuunga mkono kaulimbinu ya Tanzania ya viwanda, kampuni hiyo imeamua kujenga kiwanda kingine cha kuchambua pamba wilayani Meatu.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Shinyanga kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

No comments:

Post a Comment