Monday, 23 July 2018

Rais Magufuli Amwagiza Mweka Hazina Kuyafuta Mashirika Yasiyotoa Gawio Serikalini

Rais John Magufuli amemwagiza Msajili wa Hazina, Dk Athuman Mbuttuka kubadilisha uongozi au kufuta kampuni, wakala, taasisi na mashirika ya umma ambayo yatashindwa kutoa gawio kwa Serikali.

Ameyasema hayo leo Julai 23, 2018 katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere wakati akipokea gawio la Sh736.36 bilioni kwa mwaka 2017/18 kutoka kwa kampuni 43 kati ya 90 ambazo zinastahili kulipa gawio serikalini.

“Halipendwi shirika, inapendwa pesa tunachotaka ni gawio na si vinginevyo. Hatutaki kuwa na kitu ambacho hakishiriki kujenga uchumi wa nchi hii, nakuagiza msajili wa Hazina (Mbuttuka) hakikisha mashirika na taasisi zote zenye kutoa gawio kwa Serikali zinafanya hivyo,” amesema Rais Magufuli

Aidha ameyapongeza mashirika ambayo hayakuwahi kutoa gawio awali na mwaka huu yamejitokeza na kuchangia katika pato la Serikali yakiwemo yale ya UTT, DSE na Kadico.

Hata hivyo, ameonya kuwa bado kuna kampuni nyingi zinazalisha kiasi kidogo ikilinganishwa na kile kilichowekezwa na Serikali, hivyo kuwataka viongozi wa kampuni hizo kujitathmini.

Pia, Rais Magufuli ametoa wito kwa kampuni za Serikali kuhakikisha zinatekeleza majukumu ipasavyo ili kuondoa mianya ya rushwa na upotevu.

“Wakati mwingine tunaliwa kutokana na uzembe wa watendaji wetu, wanakaa pale wanakuwa sehemu ya kuwaumiza Watanzania badala ya kutekeleza majukumu yao. Nawaagiza wenyeviti wa bodi na watendaji wa Serikali mkalisimamie hili. Nataka kuona matrilioni na si mabilioni kama nilivyoona mwaka huu,” amesema Rais Magufuli.

No comments:

Post a comment