Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewasihi wakazi wa kata ya Mawenzi mjini Moshi, kumchagua mgombea udiwani wa CCM, Apaikunda Naburi kwa maelezo kuwa atakuwa kiunganishi sahihi kati yao na Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Polepole ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 20, 2018 katika viwanja vya kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata hiyo, ambayo awali diwani wake, Hawa Mushi alikuwa akitokana na Chadema.

Hawa aliyechaguliwa kuwa diwani mwaka 2015 alifariki dunia mwezi uliopita na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo, sambamba na kata zingine 76 nchi nzima.

Polepole amesema maendeleo yanayoonekana katika mji wa Moshi yanatokana na sera nzuri za Serikali ya CCM, ambayo ndio imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa asilimia 80.

Katibu huyo amesema kitakwimu, halmashauri ya manisapaa ya Moshi ina uwezo wa kukusanya mapato ya ndani yanayofikia zaidi ya Sh5 bilioni wakati bajeti kwa mwaka mzima ni Sh46bilioni.

"Hawa wenzetu (Chadema) wanasema wao ndio wameleta haya maendeleo mnayoyaona hapa Moshi. Nataka niwaambie leo, halmashauri mapato yake ni Sh5bilioni kwa mwaka lakini bajeti nzima ni Sh46 bilioni. Mwenye macho haambiwi tazama,"amesema Polepole.

Polepole aliwaomba wakazi wa kata hiyo kumchagua Naburi akisema ndio chaguo sahihi la kuwaletea maendeleo wananchi wa Moshi, ikiwamo kuboresha huduma katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

Mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel amesema ni upotoshaji mkubwa kudai  Rais Magufuli hapendi vyama vya upinzani wakati anaendelea kutoa ruzuku ya kila mwezi kwa Chadema ambacho kinajinasibu kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Dk Mollel alikuwa mbunge wa Siha kwa tiketi ya Chadema kati ya Novemba 2015 hadi Desemba 2017, kabla ya kujiuzulu na baadae kuteuliwa na CCM kugombea ubunge jimbo hilo hilo na kushinda.

Kwa mujibu wa Dk Mollel, Chadema imekuwa ikipatiwa ruzuku ya Sh337 milioni kwa mwezi kwa fedha za Serikali ya CCM hivyo si sahihi kudai Rais Magufuli hapendi upinzani.

Dk Mollel amedai pamoja na chama hicho kupokea mamilioni hayo ya fedha kwa mwezi, kimeshindwa kuzitumia kwa maendeleo ya chama hicho na ndio maana hadi leo hakina ofisi yake ya kujenga.

Katika mkutano huo, CCM kiliwatumia makada wa zamani wa Chadema waliohamia CCM, kuwashawishi wakazi wa kata ya Mawenzi, kumchagua mgombea wa CCM.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: