Monday, 16 July 2018

Ngassa azungumzia kuzushiwa kifo


Mchezaji mpya wa klabu ya Yanga Mrisho Ngassa, ameeleza kusikitishwa na taarifa zilizosambazwa mitandaoni kuwa amefariki dunia wakati yeye ni mzima na anaendelea na ratiba za maisha yake ya kila siku.

Baada ya Ngassa kukanusha taarifa hizo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, www.eatv.tv ikamtafuta ili kujua taarifa hizo amezichukuliaje na anahisi kwanini zimeandikwa ndipo akadai zimemuumiza sana yeye, familia na marafiki zake.

''Nimeumizwa sana na sijui kwanini huyu mtu kaandika lakini tumsamehe tu ila ajue tu amewashtua wazazi wangu na mimi pia mpaka sasa napoongea nipo na watu baadhi wamefika kutaka kujua ukweli kama nipo hai'', - amesema.

Mtumiaji mmoja wa mtandao wa 'Facebook' anayetumia jina la Christopher Paul alipandisha taarifa inayoelezea kuwa mchezaji huyo amefariki leo katika hospitali ya taifa Muhimbili kwa tatizo la shinikizo la damu.

Jana Julai 14, Mrisho Ngassa alitambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa klabu ya Yanga akiwa amesajiliwa kutoka katika klabu ya Ndanda FC ya Mtwara ambayo aliichezea msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment