Friday, 13 July 2018

Nahodha wa timu ya Taifa ya Croatia Adai MATUSI na DHARAU Ziliwaponza England Wakajikuta Wanapigwa 2-1

Nahodha wa timu ya Taifa ya Croatia, Luka Modric, amesema kilichowasaidia wao kuing’oa England katika nusu fainali ya Kombe la Dunia ni dharau.

Modric anayeichezea Real Madrid ya Hispania, alisema kuanzia wanahabari, mashabiki na wachezaji wa England ‘Three Lions’, waliidharau Croatia jambo lililowapa mwanya wa kuifunza adabu kwa kuichapa 2-1.

Licha ya England kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 lakini iliruhusu bao la kusawazisha kwa Croatia na baadaye wakajikuta wakiishiwa nguvu katika dakika 30 za nyongeza ndipo mkongwe Mario Mandzukic alipowafunza adabu kwa kupachika bao la ushindi.

“Naweza kusema vyombo vya habari na wachambuzi wote wa soka wa Uingereza waliiponda na kuidharau Croatia, waliwapamba wachezaji wao mpaka wakatuona kama wanasesere, hili ndilo lililotufanya tushinde mchezo huu,” alisema Modric.

Alibainisha kuwa matusi na dharau hizo ndizo zilizowasukuma wao kucheza kwa bidii hadi kufanikiwa kuing’oa England katika mchezo huo.

Kwa upande wake Kocha wa Croatia, Zlatko Dalic, amewapongeza wachezaji wake chini ya uongozi wa Luka Modric, kupambana na kuweza kuitoa England kwa kichapo cha mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment