Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameliagiza Jeshi la Polisi wilaya ya Tarime mkoani Mara kumkamata na kumfungulia mashtaka Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wa Wilaya hiyo, Newton Mongi na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Richard Tiboche.

Kwa tuhuma za kuitukana serikali na kuchochea mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi ya Serengeti na vijiji jirani.

Dkt Kigwangalla ametoa agizo hilo jana majira ya saa tatu usiku baada ya kuhitimisha ziara yake wilayani humo iliyolenga kutafuta suluhu ya mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa kuhusu mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji jirani ikiwemo kijiji cha Kegonga.

Akiwa njiani kwenye gari la wazi baada ya kukagua eneo hilo la mpaka kwa zaidi ya masaa sita, Waziri Kigwangalla na msafara wake walikuta lundo la mawe kwenye barabara inayotoka ndani ya hifadhi hiyo majira ya saa tatu za usiku, hali iliyosababisha taharuki kubwa na msafara wake kushuka na kuanza kuondoa mawe hayo ili kupata njia ya kupita.

Wakati zoezi hilo likiwa  linaendelea, Kiongozi huyo wa UVCCM alisikika akiituhumu Serikali kwa kuweka mawe hayo na kwamba hayakuwekwa na wananchi wa eneo hilo kama ambavyo imewahi kuripotiwa awali, jambo lililozua mshangao mkubwa  kwa viongozi wa Serikali waliokuwepo katika msafara huo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.

Mkuu huyo wa mkoa alisema tukio hilo sio la mara ya kwanza na kwamba limewahi kuripotiwa mara nyingi na uongozi wa hifadhi hiyo kuwa wananchi wa vijiji jirani hujaza mawe barabarani kwa ajili ya kuzuia magari ya doria ili waweze kulisha mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema hata msafara wa tume ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda iliyoundwa na CCM hivi karibuni kufuatilia mgogoro katika eneo hilo nao ulizuiliwa kwa mawe barabarani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: