Rais wa Marekani Donald Trump Ijumaa amekutana kwa dakika 80 katika ofisi ya Oval na Jenerali ambaye amemuelezea kama ni mtu wa pili mwenye madaraka ya juu kuliko wote nchini Korea Kaskazini.

Baadae, Trump amewaambia waandishi waliokuwako White House kwamba mkutano wa Juni 12 huko Singapore kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, utafanyika.

Lakini, Trump alikataza kuwepo baadhi ya matumaini makubwa, akisema mkutano huo ni “mwanzo “ na mazungumzo ya hapo baadae huenda yatahitajika ili kuweza kufikia makubaliano na Pyongyang juu ya kuondosha silaha zake za nyuklia.

“Sio kwamba tutakwenda katika mkutano na kusaini kitu fulani Juni 12, na wala hatukutaka iwe hivyo,” amesema. “Tutaanza kwa pamoja mchakato fulani.”

Trump aliweka wazi kuwa “hajawahi kusema kuwa hilo litafanyika katika mkutano mmoja,” lakini mchakato huo “ hatimaye utakuwa wenye mafanikio.”

Alipoulizwa na VOA iwapo Korea Kaskazini imekubali kukamilisha, uhakiki na kutositisha kuondolewa kwa silaha za nyuklia, Trump alijibu kuwa “tumezungumzia masuala mengi sana.”

Rais amemwambia Kim Yong Chol, mkuu wa zamani wa idara ya usalama katika jeshi la Korea Kaskazini, “chukua muda wako. Tunaweza kwenda haraka. Na tunaweza kwenda polepole.”

Rais ameweka wazi kuwa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitaondolewa, mpaka pale nchi hiyo itakapokubali kuacha kutengeneza silaha zake za nyuklia.

Wakati mazungumzo juu ya mkutano wa Singapore yakijadiliwa, baadhi ya wafuatiliaji wa suala hili wanahisi kuwa Trump na Kim Jong Un kila moja anajua kiuhakika kile ambacho wanataka hatimaye kukifikia.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: