Na Rachel Mkundai, Morogoro
Jumla ya wafanyabiashara wadogo wadogo 17,601 waliokuwa katika sekta isiyo rasmi mkoani Morogoro wametambuliwa na hivyo watapatiwa vitambulisho maalumu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waweze kufanya biashara zao bila kusumbuliwa. 

Hayo yameelezwa na Kamishna wa kodi za ndani wa TRA Bw. Elijah Mwandumbya alipokuwa akitoa maelezo mafupi kuhusu zoezi la kuwatambua, kuwasajili na kuwapatia vitambulisho maalumu wafanyabiashara wadogo wadogo walio katika sekta isiyo rasmi wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika viwanja vya Masika mjini Morogoro.


Mwandumbya amesema zoezi la utambuzi linafanyika kwa kupitia vikundi vya wafanyabiashara ambapo katika mkoa wa Morogoro vikundi 1851 vyenye jumla ya wanachama 17,601 wametambuliwa na watapatiwa vitambulisho maalumu vyenye jina na mahali wanapofanyia biashara zao ambavyo watadumu nabyo kwa miaka mitatu.

Ameongeza kuwa kati ya hivyo 1,851, vikundi 473 vimeshapatiwa mafunzo ya umuhimu wa kutambuliwa, kusajiliwa na kupatiwa vitambulisho vya TRA, na kati ya hivyo vikundi 143 vyenye jumla ya wanachama 2,324 wameshasajiliwa ili waweze kufanya biashara zao bila usumbufu.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa tunawatambua wafanyabiashara wadogo wadogo kwa idadi yao kwa ajili ya serikali kupanga mipango mizuri ya kuboresha biashara zao ziweze kuendelea na vile vile serikali iweze kuweka mipango mizuri ya kuwapatia huduma mbalimbali,”alisema Bw. Mwandumbya.

Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk.Kebwe Steven Kebwe, amesema ulipaji wa kodi ni jambo zuri sana na mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa inayofaidi matunda ya ulipaji kodi kwa kuwa na stendi nzuri ya kisasa ya mabasi ya abiria, stendi ya Msamvu.

Aidha alitoa  rai kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro kutumia fursa hii ya kujisajili na kupatiwa vitambulisho vya TRA ili mkoa uweze  kuwapatia huduma muhimu kama vile maeneo ya kufanyia biashara ikiwemo ndani ya stendi ya Msamvu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: